Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria wafunguka mateso ya usafiri Kwa Magufuli

Mbezi Pic Datamm.jpeg Stendi ya Magufuli

Wed, 21 Dec 2022 Chanzo: Nipashe

Abiria wanaosafiri kwenda mikoani hususani mikoa ya Kaskazini wamelalamikia utaratibu unaofanywa na mawakala wa mabasi kwa kukataa kuwakatia tiketi za siku mbili au tatu kabla ya kusafiri na kuwataka wafike siku hiyo hiyo ya safari.

Abiria anayetaka kukata tiketi ya siku mbili au tatu kabla ya safari anatakiwa kuongeza kiasi cha fedha ambacho hakiandikwi kwenye risiti jambo linalosababisha wengi kulanguliwa.

Wamelalamikia abiria kukatiwa kiti kimoja zaidi ya mtu mmoja huku wanaosafirisha watoto wamelalamika watoto wao kuondolewa kwenye siti njiani na kupandishwa watu wazima.

“Nataka kusafiri tarehe 22, nimeambiwa magari yamejaa hadi wiki ijayo, nimesogea pembeni nimeongea na mtu mmoja yeye kakatiwa tiketi anasema dada jiongeze utoe Sh. 10,000 utapewa tiketi ya siku unayotaka, hata kesho hawataki, wanataka uje siku hiyo asubuhi ndipo ukatiwe tiketi kwa bei halali,” alisema Neema Kimario akiyekuwa eneo la Shekilango, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mawakala wamelalamikiwa kutumia kipindi hiki cha sikukuu kujipatia kipato cha ziada kwa kuwatoza abiria nauli zaidi kinyume na bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Mmoja wa abiria aliyekwenda kukata tiketi ya kusafiri Desemba 23, mwaka huu, alisema sio kweli kwamba mabasi yamejaa, kwa sababu alikwenda tarehe 18 kukata tiketi kwa ajili ya kusafiri leo akajibiwa magari yamejaa, lakini alipokwenda jana alikuta watu wanakatiwa tiketi za siku hiyo.

“Tunawaomba LATRA wafanye uchunguzi wao wawe kama abiria wafike waombe kukatiwa tiketi, wakamate wanaolangua itakuwa funzo kuliko hivi tunavyowasikia wanasema hakuna ulanguzi nasi tukifika huku tunalanguliwa na kusumbuliwa, nimekaa kwenye foleni hapa kwenye hizi ofisi za hili basi na sijapata tiketi,” alisema.

Theodory Shayo, aliyekwenda kukata tiketi ya safari ya Desemba 23, alisema mawakala hao wanatumia njia hiyo ili wapate pesa za ziada.

“Mimi alinifuata wakala mmoja akanambia nimpe Sh. 10,000 katika kila tiketi, ili aniwekee nafasi katika gari linaloondoka Alhamisi kwa kuwa niliambiwa magari hayo yamejaa, akaniambia hayajajaa wanaepuka usumbufu kutokana na kujaza sana sasa hivi,” alisema Theodory.

Michael Msemvu alisema mabasi kuongeza bei za nauli kunawaathiri kiuchumi na kusababisha kutokula sikukuu kama walivyotarajia.

Rhoda Enea alilalamikia baadhi ya mawakala kukatisha tiketi zaidi ya moja kwa siti moja na wengine kuwasimamisha watoto na kuwapa siti hizo watu wazima licha ya kulipiwa nauli kamili.

“Nilisafirisha watoto peke yao kutoka Tanga, kufika Segera mmoja akaambiwa asimame, ile siti kumbe aliandikishwa abiria mwingine, imebidi watoto wapakatane kutoka Segera hadi Dar es Salaam, kwa kweli niliumia sana ukizingatia niliwakatia nauli kama abiria wengine,” alisema Rhoda.

Akizungumza na Nipashe Desemba 13, mwaka huu, Meneja Usalama na Mazingira wa LATRA, Geoffrey Silanda, alisema wanaendeleza jitihada za kumaliza adha ya usafiri ikiwamo kutoa leseni za muda kwa mabasi yatakayopeleka abiria mikoani na kwamba zimeshatolewa 42.

Alisema vilevile wanashirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL), ambalo limekubali kuongeza mabehewa ambayo yatapachikwa kwenye treni za kwenda mikoani ili kuongeza nguvu na kupunguza adha ya usafiri wanayopitia abiria kipindi hicho.

Wiki iliyopita TRL ilisema imeongeza mabehewa 10 kwenda mikoa ya Kaskazini na kufanya jumla kuwa 16, huku kwenda Kigoma yatakuwa 22, lengo ni kuwapunguzia wananchi usumbufu wa usafiri.

Katika eneo la Shekilango na Kituo cha Magufuli, Nipashe ilishuhudia Coaster zikiita abiria, lakini wengi walionekana kutaka kusafiri na mabasi makubwa.

Chanzo: Nipashe