Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria wa treni waliokwama Arusha, wasafirishwa kwa mabasi

JvnK9WKj.jpeg Abiria wa treni waliokwama Arusha, wasafirishwa kwa mabasi

Fri, 22 Dec 2023 Chanzo: mwanachidigital

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limelazimika kutumia mabasi kuwasafirisha abiria zaidi ya 200 waliokwama jijini Arusha kutokana na hitilafu iliyojitokeza kwenye kichwa cha treni.

Abiria hao waliokuwa wasafiri jana kwenda Dar es Salaam, wamesafirishwa kwa mabasi leo hadi kituo cha treni cha Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa abiria waliokwama Moshi ambao walikuwa wakienda Arusha. Wamesafirishwa kwa mabasi madogo ya kukodi.

Abiria waliokuwa wamekwama Arusha walilazimika kulala stesheni.

Kwa mujibu wa TRC, treni imechelewa kutokana na injini ya treni iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kupata hitilafu.

Abiria wa Arusha jana walilala stesheni jijini hapo baada ya treni hiyo kuchelewa na asubuhi ilitolewa taarifa ya abiria hao kusafirishwa kwa mabasi.

Mmoja wa abiria, Rehema Peter amesema tangu jana walitarajia kuondoka Arusha kwenda Dar es Salaam, lakini walikwama.

Naye Jumanne Ally, amesema leo asubuhi kabla ya kutakiwa kuondoka Arusha kwa mabasi, alitaka kurejeshewa nauli yake. Hata hivyo, baadaye alikubaliana na uongozi wa TRC.

Mkuu wa TRC stesheni ya Arusha, Victor Ningo amesema abiria wa Arusha wamesafirishwa kwa mabasi kwenda Moshi na waliokwama Moshi wamepelekwa Arusha.

"Kulikuwa na hitilafu kidogo kwenye kichwa kidogo cha treni, lakini pia njia ya Arusha ilikuwa na tatizo kidogo, hivyo abiria wangechelewa zaidi kufika Moshi na kutoka Moshi kufika Arusha," amesema.

Hata hivyo, amesema changamoto zote zimepatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa TRC, Stesheni ya Moshi, Getruda Masanja amesema changamoto zilizojitokeza zimepatiwa ufumbuzi na abiria wote wameendelea na safari leo.

Chanzo: mwanachidigital