Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria wa mwendokasi leo wachekelea

46686 Mwendokasi+pic Abiria wa mwendokasi leo wachekelea

Thu, 14 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Abiria wanaotumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka au mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam wamesema leo Alhamisi Machi 14, 2019 hali ya usafiri imekuwa na ahueni kwao.

Hata hivyo wamedai bado kunahitaji mabadiliko na maboresho kwenye uendeshaji wa mradi huo ambao umekuwa na changamoto mbalimbali.

Wamesema licha ya abiria kuwa wengi katika kituo kikuu cha mabasi hayo cha Kimara Mwisho, lakini mabasi hayo hayakawii kufika eneo hilo na kuwachukua kuwasafirisha maeneo mbalimbali ikiwemo katikati ya jiji.

"Leo abiria tupo wengi kituoni lakini haipiti dakika tano utayaona mabasi matupu yameongozana kuchukua abiria. Jana hali kama hii haikuwepo mambo yalikuwa mabaya nadhani wameanza kujirekebisha kidogo,” amesema Joseph Kisunga.

"Sielewi nini kilichowakuta hadi leo kumekuwa na ahueni, nahisi ule msukosuko walioupata abiria umewaibua na kutaka kujisafisha maana jana ilikuwa si mchezo kupata gari hapa, watu walikuwa wengi, lakini mabasi machache," amesema.

Kisunga amesema abiria wa Kimara ni wale wale hawapungui bali wanaongezeka na kinachotakiwa ni watendaji wa mradi kujipanga na kuweka utaratibu bora utakaowasaidia wao kupata huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.

Amesema ni vyema kukafanyika maboresho na utaratibu wa kiutendaji ikiwemo abiria wanaotoka Mbezi wapate mabasi ya moja kwa moja ili kuwaepusha na panda shuka iliyopo hivi sasa.

"Sasa hivi abiria anatoka Mbezi anashuka hapa, halafu anapanda basi jingine hapa Kimara. Hali inasababisha kuwepo mrundikano wa abiria katika kituo hiki, ndio maana basi likija tunakuwa katika wakati mgumu kwenye upandaji," amesema Kisunga.

Naye Zaina Abdallah amesema hali ya usafiri wa leo imeleta ahueni kwa watumiaji wa mabasi tofauti na siku nyingine hasa jana mambo yalikuwa magumu kwao kupata huduma hiyo.

"Leo unaona mabasi matatu yanafuatana na yakiwa matupu jana au siku zingine ni nadra kuona hivi. Siku zilizopita mabasi yakifika hapa yameshajaa kwa sababu watu wanapandia njia na kugeuza nayo, lakini leo ni tofauti," amesema Zaina.

Jana hali ilikuwa mbaya zaidi kwa usafiri huo kwani abiria walikuwa wengi katika kituo cha Kimara mwisho wakisubiri usafiri.

Ugumu wa usafiri huo ulitokana na mabasi kuwa machache kuliko idadi ya abiria waliokuwapo kituoni hapo.

 Soma zaidi>> Wakazi Kimara walazimisha basi la Udart kupakia abiria



Chanzo: mwananchi.co.tz