Dar es Salaam. Abiria Mwanaidi Said (83), aliyekuwa amepanda basi la Kampuni ya Saratoga akisafiri kuelekea mkoani Tabora, amefariki dunia leo alfajiri akiwa ndani ya basi hilo lililokuwepo kituo cha mabasi cha Ubungo kabla ya halijaanza safari.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Mussa Taibu ameliambia Mwananchi leo Jumapili, Juni 23, 2019 kuwa abiria huyo amekutwa na mauti akiwa ameketi kwenye kiti cha basi hilo linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kigoma kupitia mkoani Tabora.
“Alikuwa akisumbuliwa na saratani na alikuwa anakwenda mkoani Tabora baada ya kumaliza matibabu yake hapa Dar es Salaam na vyeti vimeonyesha hivyo,” amesema Kamanda Taibu.
Faida Paul ambaye ni mtoto wa Mwanaidi aliyeambatana naye katika safari hiyo, amezungumza na Mwananchi na kusema kuwa mama yake alikuwa mgonjwa na alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
“Leo tulikuwa tumeanze safari kurudi Tabora baada ya kukamilisha taratibu zote na tulikuwa tukisubiri muda tu wa kuondoka. Wakati tunasubiri muda wa kuondoka, ndiyo yakatokea ya kutokea kwa mama kufa,” amesema Faida.
Kwa mujibu wa Faida, msiba huo upo Kigamboni na maziko yanafanyika leo.