Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yarejesha safari Songea

138675c82fb88b237b9c4115ffc2523d ATCL yarejesha safari Songea

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limerejesha safari za usafiri wa anga mkoani Ruvuma baada ya kukamilika ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Ruhuwiko mjini Songea.

Serikali ilitoa zaidi ya Sh bilioni 37 kukarabati kiwanja cha ndege Songea na kuwezesha ndege aina ya Bombardier Q400 kuanza tena safari zake za kuruka na kutua katika kiwanja cha ndege cha Songea kuanzia Februari 17, mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kushuka kwenye ndege ya shirika hilo katika safari ya kwanza ya Bombadier kwenye uwanja wa Songea, Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro alisema kuanzishwa kwa safari za anga mkoani Ruvuma ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

“Ibara ya 58 ya Ilani ya CCM imetamka kwamba uwanja wa ndege wa Songea utajengwa, Ilani imetamka kwamba zitanunuliwa ndege 11 mpya, pia Ilani imetamka kuwa ATCL itaongeza safari za ndege kutoka viwanja vinne mwaka 2015 hadi viwanja 13, mwaka 2021, Songea ni kiwanja cha 13,” alisema Ndumbaro.

Alisema uwanja huo utafungua anga la mkoa wa Ruvuma na kuruhusu wawekezaji na watalii kufika Ruvuma kujionea fursa za uwekezaji na utalii, hivyo kuchangia pato la taifa na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Mgema alimpongeza Rais John Magufuli kwa kutoa Sh bilioni 37 zilizokamilisha ujenzi na ukarabati wa uwanja huo.

Meneja uwanja huo, Jordan Mchami alisema safari za ndege za ATCL zimerejeshwa mkoani Ruvuma kwa kuanzia safari kutoka Dar es salaam hadi Songea ambazo zitakuwa siku za Jumatano na Jumapili.

“Ndege itakuwa inaondoka Dar es salaam saa 1:00 asubuhi itafika Songea saa 2:25 asubuhi, itaondoka Songea 2:50 asubuhi itafika Dar es salaam saa 4:10 asubuhi, kwa kuanzia nauli ni Sh 252,000 kwenda na kurudi ni Sh 372,000, natoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani kutumia ndege hii,’’ alisema Mchami.

Uwanja wa ndege wa Songea ulijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 na uliwekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote ya masika na kiangazi.

Chanzo: habarileo.co.tz