Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

A-Z maandamano ya machinga Mwanza

MAANDAMANO DSF A-Z maandamano ya machinga Mwanza

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga wameandamana katika mitaa mbalimbali jijini Mwanza jana huku baadhi yao wakipopa kwa mawe maduka na kupora mali.

Maandamano hayo yaliyodumu kwa dakika zisizozidi 15 yalianza Saa 4:30 asubuhi leo Jumatano Februari 8, 2023 na kusababisha shughuli za kijamii na kiuchumi kusitishwa kwa muda katika barabara za Kenyatta, Nyerere, Station na Lumumba huku baadhi ya waandamanaji wakipaza sauti kupinga kuondolewa katikati ya jiji na madai ya mgambo wa jiji kuchukua bidhaa zao bila kuandikisha taarifa za wamiliki, kiwango na thamani ya mali.

Mwananchi imeshuhudia baadhi ya waandamanaji wakipora mali, hasa nguo zinazotundikwa kwenye midoli nje ya maduka.

Mali ya Wamachinga wanaotembeza bidhaa zao kwenye mikokoteni na kwa kubeba mikononi nayo ilikwapuliwa na waandamanaji hao ambao wengi walikuwa vijana wa jinsi ya kiume.

Ingawa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Selemani Sekiete amesema ofisi yake haifahamu kiini cha maandamano hayo, mfanyabiashara eneo la Makoroboi katikati ya Jiji la Mwanza, Ezekiel John amehusisha tukio hilo na operesheni ya kuwaondoa wamachinga wanaorejea katikati ya jiji.

"Jana (Jumanne Februari 7), mgambo wa jiji walifika hapa Makoroboi na kukuta Wamachinga wamerejea na kupanga bidhaa zao na wakaondoka bila kuwaondoa. Leo asubuhi tumefika na kukuta idadi kubwa ya mgambo wakifanya doria eneo hili na ghafla likajitokeza kundi la vijana wakaanza kuwarushia mawe huku wakipora mali ikabidi tufunge maduka,” amesema Ezekiel.

Vurugu hizo zimekoma baada ya magari ya doria na askari polisi wanaotembea kwa miguu wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa kuingia mitaani.

Juhudi za kumfikia Kamanda Mutafungwa kwa ufafanuzi hazijafanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa huku ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa pia haukujibiwa.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma) Mkoa wa Mwanza, Mohammed Dauda amesema hafahamu sababu za maandamano hayo huku akiwaomba viongozi wa Serikali katika ngazi zote kuanzia wilaya na mkoa kuchukua hatua kumaliza mivutano ya mara kwa mara kati ya wamachinga na mamlaka za Serikali.

Ametaja miongoni mwa mapendekezo muhimu ya wamachinga yaliyowasilishwa serikalini ni kundi hilo.

"Tayari tumewasilisha mapendekezo serikalini kuhusu namna ya kumaliza mivutano hii; moja ni mpango maalum wa kutenga maeneo yanayofikika kirahisi na wateja ikiwemo mitaa ya Makoroboi, Sahara na Miti Mirefu. Tunasubiri maamuzi ya Serikali,” amesema Dauda

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamachinga Mkoa wa Mwanza (MWM), Said Tembo ameziomba mamlaka husika kufanyia kazi madai ya baadhi ya mgambo kukamata na kuondoka na mali za wamachinga bila kuweka kumbukumbu ya wamiliki, kiwango na thamani ya mali inayochukuliwa.

liomba kufanyike vikao vya mara kwa mara kati ya viongozi wa Serikali na wawakilishi wa Wamachinga kutatua kero zinazojitokeza katika utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapanga wafanyabiashara hao.

“Kuna matatizo ambayo viongozi wanatakiwa kuyashughulikia kwa haraka ili kulinda nia njema ya Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapanga Wamachinga. Hili la baadhi ya mgambo kupora mali za Wamachinga ni moja ya mambo ya msingi ya kufanyiwa kazi kwa haraka kwani siyo maelekezo ya mamlaka, bali ni utashi binafsi ya wahusika,” amesema Tembo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Selemani Sekiete amesema ofisi yake siyo tu hafahamu sababu za maandamano hayo, bali pia haijapokea madai ya baadhi ya mgambo kuchukua mali za wafanyabiashara bila kuandikisha majina ya wamiliki, kiwango na thamani ya mali inayokamatwa.

“Niko nje ya ofisi muda huu, lakini hatuna taarifa ya malalamiko ya mgambo kuchukua mali za wafanyabiashara bila kuweka kumbukumbu ya wahusika, kiwango na thamani ya mali; labda uwasiliane na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya (Nyamagana) kwa sababu nayo inafuatilia kwa karibu masuala ya wamachinga,” amesema Sekiete

Juhudi za kumpata Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makiligi hazijafanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kujibiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live