Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

6 wajeruhiwa baada ya dari la ofisi kuporomoka

8fa6b9f4e645ccc2ed905bf226f7a3cc.jpeg 6 wajeruhiwa baada ya dari la ofisi kuporomoka

Mon, 14 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU sita wamejeruhiwa akiwemo mjumbe wa serikali za mtaa wa Tupendane, kata ya Manzese, manispaa ya Ubungo baada ya dari la ofisi walimokuwa wakifanyiakazi kuporomoka.

Mjumbe huyo, Sophia Mgaya alikimbizwa hospitali kwa matibabu baada ya kujeruhiwa kichwani na mkononi.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ubungo, Beatrice Dominick, dari la ofisi hiyo liliporomoka jana mchana kutokana na uchakavu.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema walisikia kishindo kikubwa na walipoingia ofisini humo walikuta watu hao wakiwa wamefunikwa na dari na kuanza hekaheka ya kuwaokoa.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Abdillahi Panzi alisema dari la ofisi hiyo limebomoka katika kipindi ambacho wameanzisha harakati za ukarabati kwani wakati alipochaguliwa alikuta ipo katika hali ya uchakavu.

"Ifahamike kwamba ni kipindi kifupi tangu mimi na wajumbe wa serikali ya mtaa tulipochaguliwa, tulipoingia tukaanza harakati za kutafuta fedha za kukarabati sasa limeporomoka," alisema Panzi.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice alisema ofisi yake itafanyia ukarabati ofisi hiyo iwe ya kisasa na kuhudumia watu wengi zaidi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz