Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

564 kukosa sekondari kwa ukosefu madarasa

2e62510272f824bff6a99792234c3a32.jpeg 564 kukosa sekondari kwa ukosefu madarasa

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI 564 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka huu kutoka halmashauri mbili mkoani Rukwa, hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza awamu ya kwanza kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa.

Hayo yalielezwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo wakati wa kutangaza uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Alitoa maagizo nane kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maofisa elimu na wazazi kuhusu uboreshaji wa elimu na kuhakikisha madarasa yanapatikana.

Alifafanua kuwa katika wanafunzi hao 564, 310 wanatoka Manispaa ya Sumbawanga na 254 Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.

"Nafahamu kuwa wanafunzi 16,540 wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza 2021 kwa awamu ya kwanza. Lakini pia wapo wanafunzi 564, kati yao wanafunzi 310 kutoka Manispaa ya Sumbawanga na 254 Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, ambao hawakuchaguliwa katika awamu hii kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa," alisema.

Alimwaagiza Mkuu wa Wilaya yaKalambo, Colors Misungwi na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfany Haule kusimamia kikamilifu upatikanaji wa vyumba vya madarasa vinavyohitajika na wanafunzi waliokosa nafasi ili kabla ya Februari 28, mwakani wajiunge na kidato cha kwanza. Kiutawala wilaya ya Sumbawanga ina halmashauri za wilaya za Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga.

"Ujenzi wa vyumba vya madarasa uwe ajenda ya kudumu kwa kila halmashauri, kwa kuwa idadi ya wanafunzi wanaondikishwa kujiunga na shule imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na mfululizo wa matokeo ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa miaka sita inaonesha ufaulu wa mkoa umekuwa ukipanda kutoka 2015 hadi 2019. Lakini 2020 ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.03 ukilinganishwa na 2019 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 81.01 wakati 2020 ufaulu umekuwa asilimia 80.03,” alisema.

Pia, aliwataka maofisa elimu kuongeza ufuatiliaji wa taaluma shuleni ili kuhakikisha walimu wanafundisha kwa kufuata mitaala.

Alieleza kuwa mkoa huo katika kata 27 hazina shule za sekondari, ambapo wilaya ya Kalambo zipo kata nane, Nkasi saba, Manispaa ya Sumbawanga mbili na Halmashauri ya Sumbawanga kumi

Hivi karibuni Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo alitangaza kuwa wanafunzi 759,706 waliofanya huo mwaka huu, wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwakani.

Chanzo: habarileo.co.tz