Jumla ya wanafunzi 5,236 ambao hawakuchagulia kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu, wamepewa nafasi za masomo ya ufundi katika vyuo 52 vya Serikali na binafsi mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, amesema hayo leo Ijumaa Februali 3, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu na jitihada za mkoa huo katika kunusuru kundi hilo kukaa mitaani hali ambayo itasabisha kujihusisha na matukio ya uhalifu .
“Kama Mkoa tulikaa na kujipanga namna ya kusaidia kundi hilo na kuona njia pekee wapate elimu katika vyuo vya ufundi stadi na binafsi kwa utaratibu maalum, ikiwepo mpango wa elimu kwa walioikosa (Memkwa) zitakazosaidia kuondoa kundi la vijana waliokosa elimu ya Sekondari mitaani,” amesema.
Homera amesema katika juhudi hizo za Serikali kuna michango kidogo ambayo wazazi watatakiwa kuchangia, ikiwepo huduma za vyuo na chakula kwa wanafunzi.
Amesema lengo la kuwawezesha wanafunzi hao ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri ikiwa ni kutekeleza maelekezo ya Serikali kusisitiza elimu ya kujitegemea kwa vijana kuacha utegemezi.
“Kupitia vyuo vya ufundi vijana watatoka na fani mbalimbali ikiwepo umeme wa magari, upambaji, mama lishe, umeme majumbani, ususi na nyingine nyingi na kwamba mara baada ya kuhitimu watapata mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri husika,” amesema.
Homera ametaja idadi ya wanafunzi watakao pokelewa katika vyuo 52 katika halmashauri za Busokelo wanafunzi 421, Chunya 80 Kyela 746 Mbarali 1,205, Mbeya jiji 661, Mbeya vijijini 1,634 na Rungwe 489.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju amesema, Serikali imetenga fedha na kutoa utaratibu hususan kwa wanafunzi wa kike waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwepo mimba kupata elimu bure.
“Kuna programu maalum ambazo zimeelekezwa na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa wanafunzi wa kike walikatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwepo mimba, kupata elimu bure ikiwepo madarasa ya elimu ya watu wazima,” amesema.
Hinju amesema kuwa kutokana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, inapoanza programu hiyo, hakuna watoto walifeli darasa la saba mwaka huu na hata wa mitaani watakao zagaa bila sababu badala yake wote wataingizwa darasani.
Akizungumzia fursa hiyo, Yasinta Joel aliyekatisha masomo kwa ujauzito, amesema mpango wa Serikali ushirikishe wazazi kupitia mikutano ya hadhara kwani kuna changamoto kwa viongozi wa ngazi za kata, mitaa na vijiji kuweka undugu zinapotokea fursa za kuilenga jamii.
“Serikali ina mipango mingi mizuri changamoto iko chini kwenye watelezaji, idadi kubwa ya walengwa kutoka familia zisizojiweza hazinufaiki, tunaomba Mkuu wa Mkoa anapozungumzia hizo fursa atambue huku chini kuna uozo,” amesema.