Jumla ya wanafunzi 397 sawa na asilimia 0.73 wameshindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 mkoani Tanga kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mimba za utotoni.
Akitoa taarifa kuhusu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 na uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omari alisema kuwa kiwango hicho ni kikubwa ukilinganisha na mwaka 2019.
Alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kupata elimu,umbali wa shule pamoja na wazazi kutokuwa na utayari wa uchangiaji wa chakula cha mchana kwa ajili ya vijana wao.
“Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kushusha kwa kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 76.44 kwa mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 71.53 kwa mwaka huu,” Omari.
Aidha alisema kuwa wilaya ya Kilindi ndio inayoongoza kwa kuwa na wanafunzi 11 waliokatisha masomo kutokana na ujauzito wakati utoro wakiwa 103 ikifuatiwa na Handeni yenye mimba sita na utoro wanafunzi 36.
Aidha alisema kuwa kati ya wanafunzi 38,394 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza ni wanafunzi 36,857 ndio waliopata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza wakati wanafunzi 1,537 wakishindwa kuchaguliwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.
“Niwaagize wakurungenzi wa halimashauri kuhakikisha mpaka ifikapo Februari 28 mwaka 2021 vyumba vya madarasa viwe vimekamilika na wananfunzo wote waliobaki wawe wamesharipoti shuleni kwa ajili ya kuanza masomo,”alisema Katibu Tawala huyo.
Hata hivyo Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Tanga Willium Mapunda alisema kuwa umbali wa shule, ukosefu wa chakula cha mchana imekuwa ni miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya kielimu mkoani hapa.