Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

370 waajiriwa ujenzi Daraja la JPM

05a9742aac49dadb172bd981ac8b41ea 370 waajiriwa ujenzi Daraja la JPM

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa Daraja la Kigongo-Busisi au Daraja la JPM, umeanza kunufaisha Watanzania ambapo hadi sasa watu zaidi ya 370 wameajiriwa katika mradi huo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa Daraja hilo la JPM, lenye urefu wa kilomita 3.2, linalojengwa katika Ziwa Victoria kwa gharama ya Sh bilioni 699.

Daraja hilo linajengwa kwa lengo la kuunganisha barabara kuu ya Usagara-Sengerema. Litakapokamilika litakuwa la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki.

Waziri Mkuu alisema tayari mradi huo umeshaanza kunufaisha wananchi, kwani Watanzania zaidi ya 370 wameajiriwa katika mradi huo. Tayari daraja hilo limepewa jina la Rais Dk John Magufuli ili iwe kumbukumbu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha maendeleo nchini.

Ujenzi wa daraja hilo unafanywa na Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC). Ulianza Februari 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 2024.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa meli ya MV Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ unaogharimu Sh bilioni 89.764 na hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 70.

Majaliwa alikagua miradi hiyo ya kimkakati jana akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Mradi yote hiyo inajengwa kwa kutumia fedha za ndani.

Baada ya kukagua miradi hiyo, Majaliwa alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kwamba ujenzi huo ni mfululizo wa ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji nchini.

“Ujenzi wa miradi hii utarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi kwa sababu huwezi kupata maendeleo ya watu bila kujenga vitu. Wananchi endeleeni kuiamini serikali yenu,” alisema.

Majaliwa alisema hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miradi hiyo ni ya kujivunia, kwa sababu itakapokamilika itawawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwa urahisi.

Ujenzi wa meli ya MV Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ unatekelezwa na kampuni ya GAS Entec na Kampuni ya KANGNAM Corporation zote za Korea Kusini, zikishirikiana na SUMA JKT.

Meli ya MV Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ inatarajiwa kukamilika Desemba 2021, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa matatu na madogo 20.

Wakizungumzia kuhusu ujenzi wa miradi hiyo, wabunge wa mkoa wa Mwanza walimpongeza Rais Magufuli kwa miradi hiyo, kwamba itaboresha maendeleo ya mkoa wao.

Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti alisema hakuna aliyefikiria kama ujenzi wa Daraja la JPM ungetekelezwa. "Mradi huu ni wa muujiza, tunamshukuru sana Rais," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz