Bukoba. Abiria 24 waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Arusha Express kutoka Bukoba kuelekea Arusha wamenusurika kifo baada ya basi hilo kuteketea kwa moto leo alfajiri Mei 21, 2019 eneo Kibeta mkoani Kagera.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Mei 21, 2019 shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mlinzi wa kituo cha mafuta cha Smart Oil, Vicent Michael amesema alifuatwa kuombwa mtungi wa kuzima moto baada ya basi hilo kuanza kuteketea.
Amesema baada ya kufika lilipokuwa basi hilo alishuhudia abiria wakiwa wametelemka na kushusha mizigo yao, hivyo alianza kutumia mtungi huo kuzima moto bila mafanikio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa hakuna abiria aliyejeruhiwa na walipanda basi jingine na kuendelea na safari.
Kamanda wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Hamis Dawa amesema wamefika mapema eneo la tukio na kuwa vifaa vya kuzimia husaidia kupambana na moto wa awali na wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu jinsi ya kuepuka majanga ya moto.