Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

21 wajeruhiwa mvua yenye upepo ikibomoa nyumba 39

Mvua Yawatenga Wananchi Wa Kata Ya Maboga Na Wengine 21 wajeruhiwa mvua yenye upepo ikibomoa nyumba 39

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi 21 wa Kisiwa cha Buyanzi Wilaya ya Bunda mkoani Mara wamejeruhiwa sehemu mbalimbali ya miili yao baada ya nyumba zao kubomolewa na mvua zilizoambatana na upepo mkali.

Kufuatia tukio hilo watu hao walikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya St Mary's iliyopo Mji wa Kibara wilayani Bunda baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na matofali na miti iliyotumika kujenga nyumba hizo.

Katika tukio hilo lililotokea usiku wa Novemba 23, 2023 mbali na watu hao kujeruhiwa pia nyumba 39 zilibomolewa hivyo kupelekea kaya 27 kukosa makazi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kati ya watu waliojeruhiwa wanawake ni 11, wanaume nane na watoto wawili.

Amesema majeruhi wawili tayari wameruhusiwa kutoka hospitalini huku wengine wakiendelea na matibabu na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

"Nitoe wito kwa jamii kuchukua taahadhari nyakati hizi za mvua hasa ikizingatiwa kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa imetoa mweleko juu ya uwepo wa mvua za Elinino, wavuvi na wasafiri wanaovuka majini wazingatie usalama ikiwemo kuvaa majaketi okozi kwa usalama zaidi," amesema Magere

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema tayari Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imepeleka msada wa vyakula kwa kaya zote zilizoathiriwa na tukio hilo.

“Wakiwa wamelala usiku kuliibuka upepo mkali uliombatana na mvua na na hivyo kuanza kubomoa nyumba na kuharibu mashamba ambapo mazao yameharibika kabisa bado tunafanya tathmini kujua ni ekari ngapi zimeharibiwa,"

"Tayari nimeagiza wapelekewe chakuka ikiwemo kilo 20 za unga kwa kila kaya kwani hivi sasa hawana chakula na wanategemea malazi kwa wenzao ambao hawakupata madhara wakati huo Serikali ikiendela na taratibu zingine," amesema Dk Naano

Wakisimulia tukio hilo baadhi ya majeruhi na mashuhuda wamesema hali hiyo ilikuwa kama kimbunga ambapo miti iling'olewa na nyumba kuezuliwa paa na tofali zikiruka na kuwaagukia.

"Ilikuwa ni usiku wa manane tukaasikia upepo mkali wenye kutoa sauti ya muungurumo ukivuma nje, ghafla nikaona paa la nyumba yangu likiezuliwa mara vitu vyote ndani vikapeperushwa na tofali zikaniangukia kifuani," amesema Kitwanga Kanima ambaye ni majeruhi.

Majeruhi mwingine, Esther Mkama amesema kabla ya kulala ilianza kunyesha mvua ya kawaida lakini hali ilibadilika usiku wa maneno ambapo akiwa mwenye usingizi mzito alishtuka na kusikia upepo mkali ukiunguruma nje .

"Nikiwa bado nastaajabu nikaona ukuta wa nyumba ukibomoka nikapiga kelele na kumuamsha mume wangu, katika kuhangaika nikaangukiwa na tofali kifuani," amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live