Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

100 mbaroni wakidaiwa kuchoma nyumba, kuharibu mali

BD7F7505 A4FF 43EA B00C 1E861AA3093F.jpeg 100 mbaroni wakidaiwa kuchoma nyumba, kuharibu mali

Sat, 16 Sep 2023 Chanzo: Mwananchi

What you need to know: New Content Item (1) Kigoma. Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma linawashikilia zaidi ya wakazi 100 wa Kijiji cha Mahembe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa tuhuma za kuvamia nyumba ya mfanyabiashara na mkulima, Khalid Mwela, kuichoma moto na kufanya uharibifu wa mali zake.

Kabla ya kuwashikilia watu hao, jeshi hilo lililazimika kuwatawanya wananchi wa kijiji hicho kwa mabomu ya machozi mara baada ya kuvamia nyumba ya mfanyabiashara huyo baada ya kuwazuia watu wanaodaiwa kuwa waganga wa kienyeji maarufu kama Kamchape kutoa uchawi nyumbani kwake.

Watu hao waliokuwa wakipita nyumba hadi nyumba kwa madai ya kutoa uchawi waligonga mwamba baada ya kufika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo siku ya Jumanne, Septemba 12, 2023.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu amesema jeshi hilo linalaani vikali tukio hilo la kufanya uharibifu wa mali za watu na kwamba linaendelea na uchunguzi kuweza kubaini gharama za mali zilizoharibiwa.

Amesema Serikali haitambui kundi hilo linalodaiwa kutoa uchawi kwenye nyumba za watu na hadi kufikia sasa watu zaidi ya 100 wanashikiliwa kwa upelelezi zaidi akidai bado wanaendelea na oparesheni ya kuwakamata watu wanaojihusisha na shughuli ambazo ni kinyume cha sheria.

Mdogo wa mfanyabiasha huyo, Yusuf Ali amesema baada ya kuvamiwa, kundi hilo lilifanya uharibifu, kuchoma nyumba, kuchukua magunia 70 ya mahindi yenye thamani ya Sh7 milioni ambayo yalikuwa mtaji wake wa biashara.

“Nilienda moja kwa moja kuangalia magunia yangu ya mahindi lakini sikuweza kuyakuta yote nilikuta saba kati ya magunia 70 niliyokuwa nimeacha nyumbani kabla sijaondoka,”amesema Ali

Mke wa mfanyabiashara huyo, Rehema Khalidi amesema saa 7 mchana kundi hilo la Kamchape lilifika katika mlango wake mkubwa ambao ulikuwa umefungwa na kuanza kupiga ngoma na walipoona mlango haufunguliwi walianza kuchimba chini na kuweka vitu vinavyodaiwa kuwa ni dawa.

Amesema baada ya muda mchache kupita kundi hilo likiwa limefika nyumba ya tano kutokea hapo kwake, askari walifika eneo hilo na kuanza kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi.

Khalid amesema baada ya wananchi kutawanyika, ghafla walirudi tena na kusimama katika mlango wa mfanyabiashara huyo wakidai wabomoe nyumba na kuichoma moto jambo ambalo lilimshtua.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mahembe Kati, Dunia Ngali amesema kama Serikali ya kijiji wanalaani tukio la baadhi ya wananchi kuchoma nyumba ya mwanakijiji mwenzao na kufanya uharibifu wa mali zake.

Chanzo: Mwananchi