Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zungu: Kumchagua Waitara ni sawa na usajili wa Simba kwa Kagere

15230 Pic+waita TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu amesema kama wananchi watamchagua Mwita Waitara kuwa mbunge wa Ukonga ni sawa na Simba walivyomsajili mshambuliaji wa Meddy Kagere kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Zungu ameyasema hayo leo jioni Jumapili Septemba 2, 2018 katika mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Ukonga uliofanyika viwanja vya Masai, Kitunda.

Mbunge huyo amesema wanatambua uwezo alikuwa nao Waitara na kumlinganisha na mchezaji wa Simba Kagere anayeongoza kwa ufungaji Ligi Kuu ya Tanzania Bara akiwa na magoli matatu katika michezo miwili aliyocheza.

"Sasa fikiria hapa yupo Kagere, kule Makambo, Boni na Okwi, ukiangalia hapa ni timu iliyokamilika.”

"Nawaomba wananchi msimfanyie majarabio katika uchaguzi huu, kwani ni mtu msomi, tena wa masomo ya Sayansi, Fizikia, Hesabu na Kemia,” amesema Zungu.

"Ni mtu ambaye atawafanya mtembee kifua mbele kokote, kwani mbali ya usomi wake pia ni mchapakazi na mpenda maendeleo kwani kila akisimama bungeni anataja shule, hospitali, nani kama Waitara,?" Alihoji Zungu

Naye Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amewataka wananchi hao wawapuuze wanaomsema Waitara msaliti, kwani kumchagua kwenda bungeni ataendelea kuwaletea maendeleo ikiwemo barabara.

"Kwa taarifa yenu Kinondoni kwa sasa wamenichagua pamoja na kwamba niliambiwa nimewasiliti watu lakini ndio kwanza kumenoga hivyo mchagueni Waitara, Ukonga nako kutanoga,” alisema Mtulia aliyekuwa CUF akahamia CCM

"Hivi kumchagua kwenu Waitara mtapungukiwa nini zaidi ya kuendelea kuwaletea maendeleo aliyokuwa kajipangia kuwafanyia," amesema Mtulia.

Mtulia anaungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Tambwe ambaye amesema Waitara akiwa mbunge ni rahisi kwenda kuomba mambo ya maendeleo kwa Waziri au Rais.

Munde amesema kwa kuwa kwake CCM walikuwa kutwa wakitoka nje panapoitishwa bajeti kwa kile walichodai kususia Bunge. 

Amesema CCM ndio kinachokusanya kodi na kushikilia bajeti hakuna chama chenye kuweza kufanya kazi hiyo kwa sasa.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ alisema kwa kuwa alishakuwa katibu katika jimbo la Musoma mkoani Mara anamjua vizuri Waitara.

Amesema kitendo cha (John) Heche kuja hapa kumtukana Waitara wakipuuze kwani anajua wazi kurudi kwake CCM, atakomboa majimbo yote ikiwemo la Heche (Tarime Vijijini) na huo ndio wasiwasi wake mkubwa.

Kibajaji amesema ameona bora ahamie CCM kwa kuwa (Freeman) Mbowe akimuona anaongea na waziri wa maji kuomba maji, anamuita na kumuhoji, jambo ambalo anashindwa kuwasaidia wapiga kura wake hivyo hajafanya kosa kuhamia CCM.

“Hapa hamchagui Ilani, mnachofanya ni kumchagua mtu wa kwenda kuitekeleza tu,” amesema Kibajaji.

Amesema mgombea wa Chadema (Asia Msangi) ni sawa na kutoa mlango na kuweka pazia kwani hawezi hata siku moja kumfikia Waitara.

“Kumchagua Waitara ni kuiongezea nguvu CCM bungeni, kwani wakati wakiwa na wabunge zaidi ya 200, Chadema wana wabunge 42 jambo ambalo ni sawa na kuweka kijiko cha sukari kwenye chai iliyopo kwenye pipa,” amesema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mariam Kisanji amesema alichokifanya Waitara ni sawa na mke kuachwa kwa talaka moja na kama mnavyojua kisheria huachwa kwa talaka tatu.

"Waitara jamani bado ana nafasi kubwa, kwani pamoja na mke kuachwa baadye huwa mumewe anamrudia nini Waitara" amesema Kisanji.

Mbunge huyo aliongeza hata katika wanawake kuwachagua wanaume sasa hivi, huchagua ambaye anaweza kuilea familia na si mwanaume suruali na kwao CCM wamemchagua Waitara kwa kuwa wanajua uwezo wake na namna atakavyokisaidia chama.

Mwisho

Chanzo: mwananchi.co.tz