Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hatoshiriki kwenye uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho unaotarajia kufanyika mwezi Machi mwakani.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mnanila Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma mpakani mwa Tanzania na Burundi kiongozi huyo alisema kuwa kwake inatosha kwa sasa kugombea nafasi hiyo kulingana na katiba ya ACT Wazalendo.
Zitto alisema kuwa, katiba ya ACT Wazalendo inatamka kwamba kiongozi wa chama atakaa madarakani kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano hivyo tayari ametimiza utaratibu wa katiba na hatagombea tena nafasi hiyo ili kutimiza matakwa ya katiba na kutoa nafasi kwa wanachama wengine wa chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Kiongozi huyo alisema kuwa hana sababu ya kung’ang’ania madaraka wakati katiba inaeleza wazi na wao (ACT) kama chama ambacho kinahubiri kufuatwa kwa katiba kinatekeleza katiba yao kuonyesha demokrasi ndani ya chama inatekelezwa kwa vitendo hivyo hayuko tayari kung’ang’ania madaraka.