Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto aukacha Urais, ataka kurudi bungeni

Zitto Pic Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo anayemaliza muda wake, Zitto Kabwe amesema hatogombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, bali atagombea ubunge wa Kigoma Mjini.

Mwanasiasa huyo ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Februari 2024, akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam, baada ya kuulizwa kama atagombea urais au ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Zitto amesema kwa vyovyote vile anataka kurejea bungeni ili auimarishe mhimili huo akidai Bunge limerudi nyuma tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Wanachama wakinichagua kwamba niendelee (kumpitisha kuwa mgombea ubunge) nitagombea ubunge kwa sababu mimi kwa vyovyote vile nataka nirudi bungeni kwa sababu naamini kwamba miaka hii mitano ambayo hatukuwa bungeni Bunge limerudi nyuma,” amesema Zitto na kuongeza:

“ kuna matatizo kadhaa huwezi kulilaumu Bunge kwa ujumla wake lakini tunafahamu ni Bunge ambalo limetokana na mchakato wa uchaguzi ambao haukuwa wa kidemokrasia. Kwa hiyo tungependa kulirejesha Bunge lile kabla ya 2015 ili tuweze kutengeneza mazingira bora zaidi.”

Zitto amewahi kuwa mbunge wa Kigoma  katika vipindi tofauti ambapo 2005 alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, hadi 2020 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live