Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto asisitiza wapinzani wawe na mgombea mmoja

347577cb528a94654c0cb6cb11222ffa Zitto asisitiza wapinzani wawe na mgombea mmoja

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto amesema Watanzania hawatavisamehe vyama vya siasa vya upinzani iwapo havitamsimamisha mgombea mmoja wa urais anayekubalika kwenye vyama hivyo.

Zitto alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa nchi ni kubwa kuliko vyama hivyo ubinafsi uwekwe kando kwa maslahi ya nchi.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya chama kuitambulisha timu ya kampeni kitaifa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Zitto alisema hivi sasa vyama vya siasa vya upinzani viko kweye mazungumzo na kwamba jambo muhimu ni ushirikiano.

“Watanzania hawatatusamehe iwapo hatutasimamisha mgombea mmoja wa urais, kwenye majimbo tuache ubinafsi tuangalie anayekubalika asimame. Tanzania ni kubwa kuliko vyama vyetu, Watanzania wanataka ushirikiano kuleta mabadiliko kwenye uchaguzi huu. Joto la uchaguzi mmeliona, watu wamechangamka wanataka ushirikiano na sio ubinafsi,”alisema.

Zitto alisema, ACT Wazalendo kinataka ushirikiano huo ndio maana wakati wa Mkutaon Mkuu wa chama hicho walipitisha kwa kauli moja azimio la kushirikiana na vyama vingine vya upinzani vilivyo makini hadi mwisho wa uchaguzi.

Alisema ana imani kwamba viongozi walioteuliwa kushiriki kwenye mazungumzo na vyama vingine watafikia muafaka mwema ili kuhakikisha wanashinda uchaguzi kwa kishindo.

Zitto alisema timu ya kampeni ya ACT-Wazalendo, inaongozwa na Mwenyekiti Joram Bashange ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara na Meneja wa Kampeni ni Emmanuel Lazarus ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Alisema timu hiyo hivi sasa ipo kwenye mchakato wa kuandaa ratiba ya kampeni na muda ukifika watatangaza lini tarehe na eneo la kuzindua kampeni za chama hicho.

“Naomba kwa sasa nisitaje ni lini tutazindua kwa sababu kuna timu inayoshughulikia hayo ambayo imeandaa utaratibu wote na ratiba hiyo inaanza wiki hii, hayo yote yatasemwa na wahusika kwa sababu tumeshawapa majukumu ya kazi hiyo,”alisema Zitto.

Chanzo: habarileo.co.tz