Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto asema hatokubali uteuzi wowote serikalini

11930 Pic+zitto KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe,

Mon, 23 Aug 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameweka wazi kuwa ikitokea akapata uteuzi wa wadhifa wowote serikalini, hataukubali, kwani kwa sasa ameweka nguvu na maono yake kwenye kujenga chama.

Zitto ametoa kauli hiyo juzi kwenye mahojiano na kituo kimoja cha luninga baada ya kuulizwa kama ataafiki uteuzi wowote kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa mshauri wa chama hicho, Prof. Kitila Mkumbo.

Akifafanua hoja hiyo, Zitto amesema: “Hapana nataka nijenge chama, huwezi kujenga taifa ukiwa na vyama goigoi, lazima uimarishe vyama vya siasa ili uwe na vyama madhubuti, vizae serikali madhubuti, kwa sasa hivi naona utume wangu siyo kuwa serikalini.”

Ameongeza: “Utume wangu ni kuijenga ACT-Wazalendo kiweze kuwa chama imara, ambacho kinaweza kudhibiti mapigo ya aina yoyote na kinachoweza kuzalisha serikali itayoweza kuhudumia Watanzania vizuri.

Nitamshukuru Rais kwa imani yake kwangu, ila nitamwomba atafute mtu mwingine atakayeweza kuifanya kazi ambayo mimi ningeweza kuifanya, ili mimi nipate nafasi ya kujenga Chama cha ACT-Wazalendo.”

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa 2020, ambao ripoti yake ilikabidhiwa juzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Zitto alidai katika hali halisi hapakuwa na uchaguzi, bali operesheni ya kuturudisha kwenye mfumo wa chama kimoja.

“Binafsi sikushindwa uchaguzi wowote, nimefanya kazi kubwa sana Kigoma kipindi chote nilichokuwa kwenye siasa na nimepandisha hadhi ya Mkoa wa Kigoma, Siyo kwamba wanaKigoma walinikataa. Ninaamini wapo wanaCCM wenye uwezo mkubwa ambao wangeshinda kihalali vilevile kama uchaguzi usingevurugwa,” alisema Zitto.

Akijibu swali kuhusu tofauti ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na utawala uliopita, Zitto alisema kuna baadhi ya mambo Rais Samia mebadilisha, alitolea mfano uhuru wa vyombo vya habari.

Zitto aliongeza kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo taifa lilitegemea yabadilike ila bado yako vilevile.

Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa vyama vya siasa kukutana na Rais Samia kujadili namna ya kufanya siasa za hoja ili kuwe na mwelekeo mzuri.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz