Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto amng’ata sikio Rais Samia kimtindo

Samia Na Zitto Zitto amng’ata sikio Rais Samia kimtindo

Thu, 20 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemkumbusha Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anatekeleza kile alichokiahidi siku 109 zilizopita kwa kuhakikisha anawaunganisha wananchi wote na kuleta utulivu wa kisiasa.

Zitto alimweleza Rais Samia katika utawala wake anaweza kufanya kila kitu katika nchi hii, “ukajenga madaraja, viwanja vya ndege, bandari,” lakini kikubwa ni kuishi katika 4R alizoziahidi.

4R hizo (Reconcilation - maridhiano, Resiliency - ustahamilivu, Reforms -mabadiliko na Rebuilding - kujenga upya), Zitto alizozungumzia jana katika mkutano wa hadhara wa Rais Samia uliofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma zilielezwa na mkuu huyo wa nchi Julai 1 mwaka huu katika makala yake maalumu ya kuadhimisha miaka 30 ya vyama vingi vya siasa.

Katika makala hiyo, Rais Samia aligusia masuala mbalimbali na kueleza katika utawala wake ulioingia madarakani Machi 19 mwaka jana baada ya kifo cha Rais John Magufuli, atahakikisha anaishi kwenye 4R hizo.

Kupitia makala hiyo, Rais Samia alieleza katika kujenga Tanzania bora na anatamani jamii yenye maridhiano na maelewano.

“Ninatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote. Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote,” inaeleza makala hiyo.

Jana, Zitto aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini kwa nyakati tofauti, alikuwa miongoni mwa viongozi wanasiasa waliohudhuria mkutano huo na kupewa fursa ya kuzungumza.

Alisema juhudi zinazofanywa na Rais Samia katika kuwaleta Watanzania pamoja bila kujali itikadi zao zinaonekana, huku akieleza hata uwepo wake yeye katika mkutano huo ni moja ya ishara hizo.

Pia, alisema utendaji wake hauangalii vyama vya siasa vya watu, bali Watanzania kwa pamoja.

“Kazi ambayo umeifanya tangu uingie madaraka au kwa kukutana na vyama vya siasa kimoja baada ya kingine kupitia viongozi wao au kupitia kikosi kazi kilichoundwa kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kuboresha siasa zetu, hali ya siasa nchini imekuwa ya utulivu sana,” alisema Zitto.

Alisema utulivu huo unasaidia kuchochea juhudi za maendeleo, kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kuifanya nchi kuendelea isipokuwa njia anayopita katika kujenga maridhiano ya kitaifa, huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza na kumshukuru kwa niaba ya viongozi wote wa kisiasa nchini.

“Ninakuomba uendeleze juhudi hizi, nitumie fursa hii kukuomba sana, usiache juhudi hizi za mageuzi ya kisiasa,” alisema Zitto, ambaye ni mjumbe wa kikosi kazi.

“Unaweza kufanya kila kitu katika nchi hii, ukajenga madaraja, viwanja vya ndege, bandari lakini vizazi na vizazi vitakukumbuka kwa mawazo, hiki ambacho unakifanya na kile ulichoeleza katika 4R ni katika kueleza namna gani na dhamira yako uliyonayo ya kuifanya nchi kuwa moja na hiki ndiyo Watanzania watakukumbuka daima,” alisema Zitto na kuwaomba wanakigoma kumpokea Rais Samia ili wafanye naye kazi.

“Mama huyu hapa mpokeeni, tufanye naye kazi, tushirikiane naye tulete mabadiliko katika nchi,” alisema Zitto.

Akijibu alichokisema Zitto, Rais Samia alisema alikuwa akimsikiliza kwa makini ili ajue atasema nini, lakini mwisho wa maneno yote akamkabidhi (Rais) kwa wananchi na kutaka wampokee.

“Hiyo ikiwa na maana kuwa yale yaliyokuwa yakisemwa kabla, yaani maendeleo kwa wananchi waliyokuwa wakipigia kelele sasa yanafanyika na kelele zimehamia upande mwingine,” alisema Rais.

“Uzuri huko kwenye siasa tumewapa kazi wao wenyewe wazungumze walete mapendekezo yale yanayotekelezeka tuyakubali na yatekelezwe.”

Kauli ya Zitto ya kumtaka Rais atumie 4R ameitoa ikiwa ni siku moja imepita tangu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kusema mikutano ya vyama vya siasa ina afya ya kidemokrasia kwa Taifa.

Nape, aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, alitoa kauli hiyo ikiwa ni zaidi ya miaka sita tangu Serikali ilipopiga marufuku mikutano hiyo, ikiacha ile ya wabunge na madiwani katika maeneo yao.

Hatua hiyo ilizua malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa demokrasia, wakisema Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa imekiukwa na kuitaka Serikali iondoe zuio hilo, jambo ambalo halikutekelezwa hadi sasa.

Baada ya kelele za mara kwa mara, Desemba 15 mwaka jana, wakati Rais Samia akifungua mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini, miongoni mwa aliyoyaeleza ni suala la mikutano hiyo na uwezekano wa kuiruhusu baada ya kupata maoni ya wadau.

Aliwataka wadau wajadili na kuja na mapendekezo ya kufanya mikutano hiyo, akisema, “vyama mna haki ya kikatiba kufanya mikutano, kunadi sera zenu lakini mnaivunja wenyewe, hakuna atakayekubali anaongoza nchi anatoa kibali mfanye mkutano mnapita kuvunja magari ya watu na kufanya vurugu.”

Chanzo: mwanachidigital