Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto aeleza sababu tano wabunge wa upinzani Tanzania kung’ara uchaguzi 2020

Video Archive
Mon, 2 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa wabunge wa upinzani waliokuwa na hofu ya kurudi bungeni, angalau kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anaweza kuwatoa hofu.

Anasema mwaka 2020, kuna uwezekano mkubwa kwa upinzani kuongeza idadi ya wabunge baada ya mafanikio ya mwaka 2015.

Akizungumza na Mwananchi, mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali, ambayo alidai haiwagusi moja kwa moja wananchi, ni miongoni mwa tiketi zitakazowafanya wapinzani kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema mambo mengine yatakayowapa ushindi wapinzani ni ukata unaowakabili Watanzania wengi, kuminywa kwa haki, wapinzani kuachiana majimbo pamoja na historia ya wabunge wa upinzani kuongezeka kila unapofanyika Uchaguzi Mkuu.

Alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika juzi katika ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Alibainisha kuwa zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, haliwezi kuwa kikwazo katika uchaguzi huo.

“Sina shaka na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa sababu mazingira ya sasa ni mazuri zaidi kuliko 2015,” alisema Zitto ambaye amewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema.

Katika hoja yake ya kwanza, Zitto aliitaja miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege na mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge kuwa haimgusi mwananchi moja kwa moja.

“Wananchi wanataka kuona katika maeneo yao kuna maji, huduma za afya na shule,” alisema Zitto.

“Wabunge wengi hawana cha kueleza katika majimbo yao maana fedha za maendeleo haziendi. Kama mbunge umeshindwa kujikita kwenye sekta binafsi, huwezi kuwa na uwezo wa kuonyesha tofauti wakati ulipochaguliwa mwaka 2015, ilivyo sasa na kuelekea 2020.

“Mwananchi wa kawaida anampima mbunge kuanzia siku aliyomchagua. Anaweza kujiuliza jimbo halikuwa na maji mwaka 2015 na kama 2020 itafika maji hakuna atapima mwenyewe. Kama mwaka 2015 hakukuwa na soko na hadi uchaguzi ujao unafika soko hakuna, pia atapima.”

Alisema jambo hilo ndio litawaangusha wabunge wengi wa CCM kwa kuwa hawatakuwa na la kusema katika majimbo yao.

“Serikali inaweza kuwa imefanya miradi mingi yenye maana na ya kimkakati, lakini imekosa maarifa ya kuunganisha miradi hiyo ya vitu na maendeleo ya watu,” alisema.

“Ni suala la maarifa tu kumfanya mwananchi aamini miradi hii inayofanyika inamgusa yeye moja kwa moja.”

Akitoa mfano mradi wa ujenzi wa reli, Zitto alisema badala ya Serikali kutumia malighafi kutoka nje kwa ajili ya ujenzi huo, ingewekeza katika mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Liganga na Mchuchuma ili kutumia malighafi zitakazopatikana nchini.

“Kwa kufanya hivyo Serikali ingetengeneza ajira nyingi. Unaweza kujiona unafanya jambo ili mradi uone reli, lakini wananchi wasione chochote,” alisema.

 

Upinzani unakua tangu 1995

Hoja ya pili ya Zitto ni mwenendo wa upinzani tangu kurejea kwa uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.

Zitto alisema takwimu za kuanzia kipindi hicho ni nzuri zaidi kwa wapinzani kuliko CCM.

Alisema kati ya mwaka 1990 hadi 2015, hata kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, asilimia 70 ya wabunge hushindwa katika chaguzi, kubainisha kuwa katika kila wabunge 100, wabunge 30 ndio hushinda.

“Wabunge wengi wa upinzani huwa wanarudi bungeni ila wabunge wengi wa CCM huwa hawarudi,” alisema.

“Mfano mwaka 2005 nikiwa Chadema tulishinda wabunge watano tu wa kuchaguliwa. Nilishinda mimi (Zitto), Chacha Wangwe (marehemu), Philemon Ndesamburo (marehemu), Dk Wilbrod Slaa na Said Arfi.

“Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 tulishinda wote isipokuwa Jimbo la Tarime tu. Dk Slaa alikwenda kuwania urais ila aliyegombea kwa tiketi ya Chadema katika jimbo lake alishinda.”

Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2015, wapinzani walipata wabunge wengi zaidi huku CUF ikishinda katika majimbo 10 ya Tanzania Bara, manne yakiwa mkoani Lindi ambao una majimbo nane.

 

Haki na kipato

Zitto alisema uchaguzi ujao pia utaamuliwa na suala la haki.

“Katika haki watu watatazama matukio ya watu kutekwa. Wapo wengi waliotekwa na hadi sasa hawajulikani walipo. Watakaokwenda kupiga kura watajiuliza vichwani mwao je jambo hilo ni sahihi?” alisema.

“Wapo watakaotazama tukio la (mbunge wa Singida Mashariki, Tundu) Lissu kupigwa risasi. Serikali imeshindwa kuyaweka wazi mambo hayo. Naamini utakuwa uchaguzi mzuri na ukiwa huru na haki na wapinzani tukijipanga, CCM itaanguka.”

Pia alizungumzia kipato cha watu akisema wakati huo “mtu atatazama mfukoni kwake hali ikoje. Atajipima uwezo wake wa kiuchumi kati ya sasa na miaka mitano iliyopita ulikuwaje. Kama hali ni mbaya hatachagua chama kilichosababisha hali kuwa mbaya”.

 

Ushirikiano wa wapinzani

Alisema ili wapinzani washinde katika uchaguzi ujao ni lazima wakubali kutorudia makosa yaliyojitokeza katika uchaguzi wa 2015.

“Tangu mfumo wa vyama vingi kuanza vyama vya upinzani vimekuwa vikipata angalau asilimia 40 ya kura zote za majimbo zinazopigwa, hata kama idadi ya wabunge wanaopata inakuwa ndogo,” alisema.

“Hii maana yake ni kwamba nchi hii ni ya upinzani. Upinzani si vyama wala viongozi wa kisiasa, upinzani ni wananchi wenyewe. Ni suala la vyama vya upinzani kujipanga na kuona ni namna gani ya kufanya.”

Alisema ni lazima vyama vya upinzani kukubaliana na kuweka mgombea mmoja ili kuvuna kura nyingi.

“Uchaguzi wa mwaka 2015 vyama vya upinzani vilipoteza majimbo 48 kwa sababu ya kunyang’anyana kura. Mfano Jimbo la Segerea, Anatropia Theonest (Chadema) na Julius Mtatiro (CUF) waligombea pamoja licha ya vyama vyao kuwa katika makubaliano,” alisema.

“Kura alizopata Anatropia na alizopata Mtatiro zinazidi kura 20,000 alizopata mgombea wa CCM. Pia ACT tungeweza kushinda Kasulu Mjini kama Chadema na NCCR wasingesimamisha mgombea. ACT tungeshinda. Mbarali kama Chadema wangetuachia. NCCR wangeshinda Kasulu Vijijini kama ACT tusingesimamisha mgombea.”

Kuhusu ushirikiano mpya wa vyama vyama vya upinzani, The United Democratic Front (DeFront), Zitto alisema kwa sasa wapo katika mazungumzo na kwamba utahusisha pia makundi mbalimbali katika jamii.

“Lazima tuwe na chombo kitakachokuwa kikisuluhisha pale utakapoibuka mvutano kuhusu chama gani kisimamishe mgombea,” alisema.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz