Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto aeleza azimio litakavyoanza

34422 Pic+zitto Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya vyama vya upinzani vimeeleza mikakati itakayotumika kutekeleza azimio la Zanzibar la kuufanya mwaka 2019 kuwa wa kudai demokrasia.

Hivi karibuni, vyama sita vilikutana mjini Zanzibar na kutoa tamko lililoutangaza mwaka 2019 kuwa wa kudai demokrasia.

Viongozi wa vyama hivyo waliokutana ni pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad; Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia; Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi; Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu; Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Pamoja na mambo mengine walidai kuna mmomonyoko wa demokrasia nchini kutokana na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa.

Akifafanua mikakati ya vyama hivyo alipozungumza na Mwananchi kwa simu jana, Zitto alisema baada ya kumaliza mkutano wa Zanzibar hatua iliyofuata ni kila chama kwenda kuidhinisha tamko hilo.

“Ndani ya wiki hii kutakuwa na kikao cha viongozi wa vyama kutafakari tulipofikia kwa sababu kila chama kilitakiwa kiidhinishe tamko lile, isije ikawa ni viongozi wachache tu,” alisema Zitto.

Alisema pia walikubaliana kwenda kwa wadau wakiwamo viongozi wa dini kuwaeleza mchakato mzima waliokubaliana. “Tunazo pia hatua za kisheria na Januari 3 (kesho) tutawaeleza waandishi wa habari tulipofikia katika hatua za sheria. Vilevile tutakuwa na mikutano ya hadhara na ya ndani na maandamano.”

Alitaja miongoni mwa kazi zitakazoanza Januari hii kuwa ni pamoja na maandamano yatakayofanywa na vijana wa CUF (upande wa Maalim Seif) Januari 12, huku wanawake wa ACT Wazalendo wakifanya mkutano.

Alisema shughuli zote za mwaka wa kudai demokrasia zinaratibiwa na Maalim Seif ambaye pia anasimamia kamati ya pamoja ya vyama hivyo.

“Jana (juzi) nilikwenda gerezani kumtembelea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kupata maelekezo ya kutekeleza azimio hili,” alisema Zitto.

Alipoulizwa kuhusu makatazo yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa na Serikali kuhusu mikutano na maandamano ya vyama vya siasa, Zitto alisema, “Yote ni haramu, ndiyo maana hata viongozi wa Serikali wanapishana. Hakuna sheria inayotuzuia kufanya mikutano na maandamano. ”

Akizungumza kwa niaba ya Chadema, Mwalimu alisema shughuli zote zinaratibiwa na sekretarieti waliyoiunda na kuna kamati ya wataalamu waliyoianzisha ili kuwashauri.

“Kufanya mikutano ni haki yetu, kufanya maandamano ni haki yetu, hatujavunja sheria yoyote. Kwa mfano Chadema sasa tuko kwenye uchaguzi nchi nzima, tukifanya mikutano ya ndani wakuu wa wilaya wanawatuma ma-OCD kutukamata, ukiwauliza kosa wanasema hata wao wametumwa. Sisi hatutakubali,” alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu alifafanua kuhusu ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Tweeter akiwataka wanachama wao kupeperusha bendera usiku wa mwaka mpya, alisema ni ishara ya kuanza kutekeleza azimio la Zanzibar.

“Vilevile niliandika upepo wa demokrasia na haki uvume Tanzania nzima mwaka huu. Nilitaka wanachama wapeperushe bendera kutekeleza azimio hilo na pia kwa kuwa mwenyekiti wetu (Mbowe) yuko gerezani,” alisema Dk Baregu.



Chanzo: mwananchi.co.tz