Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto: Wapinzani hatupingi maendeleo

10745 Pic+zitto TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hakuna mpinzani anayepinga maendeleo ya nchi, lakini suala linaloleta matatizo ni namna ambavyo maendeleo hayo yanaletwa na Serikali ya CCM.

Kiongozi huyo ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa tiketi ya chama hicho uliofanyika maeneo ya Shule ya Msingi Kombezi jijini Tanga.

“Hakuna mpinzani anayeweza kusimama na kupinga shirika la ndege la taifa kufufuliwa, Reli ya kisasa kujengwa na hakuna mpinzani anayeweza kusimama kupinga nchi kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme,” alisema Zitto.

Hata hivyo, alisema hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu atakayesimama kuunga mkono namna ambavyo CCM inavyoyaleta maendeleo hayo.

Wakati huohuo kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo aliwataka wananchi wa Kata ya Makorora kukichagua chama hicho ili Tanga irudi kwenye historia yake na iondokane na siasa za kudidimiza.

Alisema kuwa Tanga inahitaji sauti ambayo itasaidia kurudisha historia ya Jiji la Tanga, hivyo wasifanye makosa kuichagua CCM kwani hakuna wanayoweza kufanyiwa na serikali hiyo.

Alisema kuwa uchaguzi huu unahitaji utulivu na si uchaguzi wenye kuwa na ushabiki ambapo aliongeza kuwa mgombea wa ACT ni bora zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine kwakuwa yeye ni kijana msomi.

Mgombea huyo wa ACT -Wazalendo, Mohamed Masoud aliwataka wananchi wa kata hiyo kumchagua yeye ili aweze kuwa kiranja wa kutatua changamoto za kata hiyo.

Alisema kata hiyo ina changamoto nyingi hivyo aliomba siku ya uchaguzi wakamchague ili aweze kuzisemea changamoto hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz