Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto: Tusibweteke kwa demokrasia ya kupewa

Zitto (600 X 337) Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo nchini

Fri, 22 Jul 2022 Chanzo: mwanachidigital

Pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha kukubali kilio cha katiba mpya, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametaka Watanzania wasibweteke ili kuepuka kurudia makosa yaliyosababisha nchi ikawa na “demokrasia ya kupewa”.

Lakini kiongozi huyo anasema ana imani na Rais Samia kuwa anaweza kuifikisha nchi sehemu nzuri, lakini akasema iwapo katiba inayotokana na madai ya wananchi itashindikana, basi angalau iwepo katiba ya maridhiano.

Zitto alikuwa akizungumza katikamahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu kumbukumbu ya miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 baada ya kufutwa mwaka 1965 wakati katiba ilipobadilishwa na kuanzisha mfumo wa chama kimoja.

“Nina imani na Rais Samia, namuona yuko tofauti na wengine. Naona tutapiga hatua. Kwanza tofauti na (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete, Samia ameagana na CCM. Chama kimeridhia, Kwa hiyo tunaweza kupiga hatua,” alisema.

“Lakini wengi CCM hawataki mabadiliko, hawataki status quo ibadilike. Mfano watu 84 hawakushinda kura za maoni wapo bungeni. Kinachotakiwa ni kumpa moyo Rais na mtu mwingine yeyote anayeonekana anataka hili.

“Mazingira ya sasa yanaweza kuwa mazuri, lakini ni muhimu tukachukua tahadhari.”

Advertisement Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini amesema katika kipindi cha miaka 30, kumekuwa na demokrasia isiyotokana na matakwa ya wananchi, bali iliyotolewa na dola.

“Uchambuzi wangu unaonyesha kwamba tumekuwa na demokrasia ya kupewa na sio inayotokana na wananchi kuidai. Hii haina maana kwamba hapakuwa na madai ya demokrasia hapana, yalikuwepo, lakini hayakuwa na nguvu,” alisema.

“Inawezekana (hivi sasa) tukawa tunaelekea kwenye demokrasia ileile ya kupewa. Kama haiwezekani hii ya kudemand (ya kuidai), basi tupate negotiated constitution (katiba ya maridhiano).”

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema anasema demokrasia ya kupewa ilitokana na CCM kuwahi madai ya demokrasia na kuteka mchakato wa mageuzi na hatimaye kubadili katiba katika kikao cha Bunge cha Aprili hadi Mei, 1992.

Awali wakati wa vuguvugu la mageuzi, kulikuwa na madai ya kuandika upya Katiba yaliyotolewa na wabunge kama Edward Ayombe Ayira, Ndembela Ngunangwa na Jenerali Ulimwengu na watu wengine waliokuwa nje kama Chifu Fundikira.

“Hii ni sifa kwa CCM kwamba iliongoza mageuzi, lakini chama tawala kikiongoza mageuzi kitaweka mazingira ya kutoondoka madarakani. Ndivyo ilivyokuwa. Wakati huo, kwa kuwa waliokuwa wanadai demokrasia walikuwa wanataka vyama vingi, mabadiliko yalipofanyika, walifurahia wakasahau mambo mengine muhimu.

“Hii ni kwamba wananchi mtakuwa na vyama lakini hamtapata hiyo demokrasia na ndicho kilichotokea mwaka 1992. Ukisoma kumbukumbu za bunge za mjadala wa mabadiliko ya nane ya Katiba mwaka huo, unaona kabisa kwamba CCM iliamua badala ya kukubaliana na madai na kuacha madai yaimarike, iliamua kuwapa wananchi demokrasia.”

Madhara ya dola na CCM kuongoza mageuzi hayo, anasema, yalianza kujitokeza mwaka 2000 wakati chama hicho kilipoanza kuvichukua vile ilivyokuwa imevitoa kwa wananchi.

“Kwa mfano uchaguzi wa mwaka 1995 hawa tunaowalalamikia wakurugenzi wa halmashauri hawakuwa wasimamizi wa uchaguzi, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya wakati huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliajiri yenyewe wasimamizi wa uchaguzi,” alisema.

Lakini, katika uchaguzi wa mwaka 2000 wakurugenzi wa halmashauri walipewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi ngazi ya majimbo, kata na mitaa, alisema.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alisema bado hiyo haikuonekana kuwa hatari kwa kuwa vyama vya upinzani viliendelea kushinda ubunge, udiwani na kushika serikali za mitaa.

“Mwaka 2015 uchaguzi ulikuwa wa ushindani sana kama ilivyokuwa mwaka 1992 na baada ya matokeo, dola ikaamua kuchukua demokrasia iliyokuwa imeitoa kwa wananchi,” alisema.

Zitto alisema kuanzia mwaka huo, wakurugenzi wa halmashauri hawakuwa viongozi kutoka serikali za mitaa waliokulia ndani ya mfumo wa utumishi wa umma, bali makada wa CCM walioanguka katika kura za maoni ndio walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Si hivyo tu, Zitto anasema, Julai 2016 mikutano ya hadhara ilipigwa marufuku, jambo ambalo halikuonekana kuwa kawaida kutokana na mazoea.

“Tulizoea ukitaka kufanya mkutano wa hadhara unatoa taarifa polisi unafanya zako, wakati mwingine hata hausubiri majibu ya polisi. Unatoa taarifa unaendelea, hiyo demokrasia ikachukuliwa,” alisema.

Mkumbo huo ulienda sambamba na wimbi la waliokuwa wabunge wa vyama vya upinzani, licha ya kushinda lakini walijiunga na CCM na mwaka 2019 sheria ya vyama vya siasa kilibadilishwa kuviondolea haki zote za msingi.

“Hatimaye tulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa wa ovyo kabisa. Tuliona wagombea wa vyama vya upinzani waliondolewa kugombea,” alisema.

Changamoto zinazoigubika demokrasia katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano, ndizo zilizosababisha wananchi kukosa mwamko wa kupiga kura mwaka 2020.

Zitto alisema ni watu 17 tu kati ya 100 waliojitokeza kupiga kura mwaka 2020, huku asilimia 12 ya vijana waliojiandikisha ndio waliojitokeza kupiga kura.

Vyama vingi si uhalisia

Zitto, ambaye aliingia siasa akiwa kijana mdogo, alisema ulifika wakati ilidhihirika kwamba mfumo wa siasa za vyama vingi upo kisheria lakini si kivitendo.

“Kwa sasa ndiyo kama vyama vimeruhusiwa upya kufanya mikutano, lakini hatari ni kwamba inawezekana tukapita kwenye njia ile ile ya demokrasia ya kupewa badala ya kwenda mbele. Sasa wananchi wadai na ziwekwe zile kanuni ili kuwe na usawa,” alisema.

Apendekeza demokrasia ya majadiliano

Zitto anasema iwapo kutakuwa na ugumu wa kupatikana demokrasia inayotokana na matakwa ya wananchi, ni muhimu ipatikane ya majadiliano yatakayohusisha makundi yote.

“Tunahitaji kufumua Sheria ya Vyama vya Siasa ili iwe inclusive. Sheria inasaidiaje vyama kuwa taasisi? Tuifanye sheria ambayo itawezesha vyama kuimarika, Tuna miaka 30 lakini kuna vyama havijawahi kupata hata serikali ya mtaa lakini vipo, kuna vilivyokua na kushuka,” alisema.

Alitaka yatengenezwe mazingira yatakayowezesha vyama vyote kuwa na uwezo wa kushika dola ili kuwe na utajiri wa watu wenye weledi wa kuongoza nchi.

“Pia kufumua Sheria ya Uchaguzi ili NEC (Tume ya Uchaguzi) iwe huru. Bajeti itatoka consolidated fund,” alisema.

“NEC iajiri watendaji wake na kuwe na inclusive process (mchakato jumuishi) wa katiba. Mazingira yamebadilika sana tangu mwaka 1977. Kwa mfano, kuna umuhimu wa kuwa na ma-DC (wakuu wa wilaya)? Kazi zao ni nini Ma-RC? Wateuliwe na Rais? Au rais apate mapendekezo kutoka RCC au Rais apelike mapendekezo RCC? Kuna umuhimu wa Rais kuteua kila mtu?”

Alisema kuna umuhimu pia wa kufumua Jeshi la Polisi ili kazi zake ziwe ni kuhudumia wananchi.

Kabwe alisema anatamani kuona mazingira ya siasa yanayompa ushindi na nafasi ya kuongoza yeyote anayeshinda katika uchaguzi.

“Yule anayeshinda apewe nafasi ya kuongoza, ningependa mazingira hayo na tulishakaribia kuyafikia japo si kwa asilimia 100 lakini tulikaribia chaguzi hazikuwa na mshike mshike,” alisema.

Mjadala wa kitaifa

Kuhusu mabadiliko ya Katiba alisema kwa kuwa ni mchakato wa kisheria kuna haja ya kufanyika mjadala wa kitaifa wa masuala yote yaliyokwaza kufanikishwa kwa ule wa awali ili kuafikiana ndiyo kuanza mchakato mpya.

Makubaliano yote, alisema lazima yapigiwe kura ya maoni ili wananchi wakubali ama kukataa na NEC ndiyo itakayosimamia.

Alisema maandalizi yake yanapaswa kutanguliwa na mabadiliko ya baadhi ya sheria ikiwemo ya vyama vya siasa na ya uchaguzi ili kama mchakato hautaisha kabla ya 2025, uchaguzi uendeshwe na chombo huru.

Alisema mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yanapaswa kuondoa mamlaka kwa Rais kuwateuwa makamishna wa NEC, badala yake nafasi hizo ziombwe kama ajira.

“Tusipoangalia, tutafika 2025 na tume hii,” alisema.

Kabwe pia alizungumzia uongozi wa awamu ya tano, akisema haukuwa wa kidemokrasia na kwamba ulikuwa ni matokeo ya uholela uliosababisha kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi.

Alisema ilifikia wakati wananchi walipenda wawe na kiongozi dikteta, na kuonya kuwa hali hiyo isijirudie.

“Siasa ni kama soko. Una bidhaa ambazo zinauzwa na kuna wanunuzi wa hizo bidhaa na chama cha siasa kinataka kipate wanunuzi wengi wa bidhaa zake, kwa hiyo kinaangalia wananchi wanataka mtu wa namna hii kinawaletea,” alisema.

“Chama kama CCM kina watu wa aina hiyo, wengi sana. Kinaweza kutuletea mtu wa aina hiyo muda wowote. Kwa hiyo tukitaka mtu aina ya Kikwete wanaleta, aina ya Magufuli wanaleta, aina ya Samia wanaleta.”

Chanzo: mwanachidigital