Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto: Kuanzia kesho Watanzania tegeni masikio

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ametuma salama za vyama vya upinzani za mwaka 2019, akisema utakuwa mwaka mgumu ambao Watanzania hawajawahi kuushuhudia kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Zitto amesema kuna maazimio waliyoyafikia katika kikao cha Zanzibar cha Desemba 16 hadi 18 kwa kukubaliana mambo mbalimbali ikiwamo kuutangaza 2019 kuwa wa kupigania demokrasia nchini kwa kufanya mikutano ya hadhara.

Amesema mwaka huo utakuwa wa kipekee na Watanzania wawe tayari kusikia kitakachokwenda kujiri.

“Mwaka unaokuja 2019 hautakuwa mwaka rahisi, utakuwa mwaka mgumu sana na utakuwa mwaka ambao nadhani Watanzania wengi hawajawahi kuushuhudia katika kipindi cha miongo miwili iliyopita,” alisema Zitto juzi jioni alipokutana na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Kikao cha Zanzibar kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni katibu mkuu wa CUF kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chadema, NLD, Chaumma, NCCR-Mageuzi na ACT- Wazalendo pamoja na viongozi wengine wa taasisi za kupigania haki za binadamu na utawala bora.

Zitto alisema, “Kufuatia kikao chetu cha viongozi tulichofanya Zanzibar, kuna yale ambayo tuliwaeleza wananchi hadharani na mengine yalibaki vifuani mwetu na tutakuwa tunawaeleza kadri muda unavyokwenda.”

Katika kusisitiza hilo, mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema, “Lakini hautakuwa mwaka mwepesi kwa nchi yetu na hautakuwa mwaka mwepesi kwa sisi viongozi wa upinzani.”

Kuhusu ACT- Wazalendo kushirikiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi, alisema hawaamini kama hilo limewezekana ndani ya mwaka huu.

“Tulikuwa hatuamini kama tutakaa meza moja na watu wa Ukawa na tunajadiliana, lakini hilo limewezekana.”

Alisema juzi mchana alikutana na Maalim Seif ambaye alikwenda katika gereza la Segerea kumtembelea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko.

“Leo (juzi) mchana nilikutana na Maalim Seif baada ya yeye kutoka kwa Mbowe, alikwenda kumjulisha kilichojiri Zanzibar lakini alinipa salamu za Mbowe kuja kwangu, huu ndio ushirikiano tunaoutaka kwa mustakabali wa Taifa letu,” alisema Zitto.

Miongoni mwa maazimio ya mkutano wa wapinzani uliofanyika Zanzibar yaliyosomwa na Maalim Seif mbele ya wanahabari Desemba 18 ni kufanya mikutano ya hadhara mwaka 2019 inayoruhusiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imezuiwa na wanasiasa wanaoifanya wamefunguliwa kesi mahakamani ama kukamatwa na kuachiwa.

Pia, Maalim Seif alitangaza kuwa Mbowe na Matiko pamoja na wanasiasa wote wa upinzani waliopo mahabusu ni wafungwa wa kisiasa na wataitangazia hivyo dunia.

“Tunatangaza sasa ni wakati sahihi na muhimu wa kuongeza umoja, mshikamano na kujitoa kwetu katika kuiendea ajenda yetu ya kitaifa ya kulinda demokrasia,” alisema.

“Tutaunda kamati ya kuratibu hatua za kuunganisha makundi ya wananchi nchi nzima na kundi lolote la wananchi, popote walipo, iwe ni wafanyakazi wanaopinga kupunjwa pensheni, wakulima wanaokosa soko la mazao yao, wavuvi wanaonyanyasika, wanafunzi wanaokosa mikopo, wanasiasa wa upinzani wanaokamatwa na polisi bila sababu watafikiwa ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kupigania haki zao,” alisema.

Pia, Maalim Seif alisema watapambana kuhakikisha Mbowe na Matiko ambao wako mahabusu pamoja na mahabusu wenzao wa kisiasa nchi nzima wapewe nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru, mbele ya mahakama na mbele ya macho ya umma.

Tamko hilo lilitiwa saini na Maalim Seif (CUF), James Mbatia (NCCR - Mageuzi), Oscar Makaidi (NLD), Salum Mwalimu (Chadema), Hashim Rungwe (Chaumma) na Zitto Kabwe (ACT - Wazalendo).

Pia, waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye walishiriki kikao hicho.



Chanzo: mwananchi.co.tz