Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zito, Sugu kuwasha moto kampeni za Chadema Tarime

10940 Zitto+pic TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anatarajia kupanda jukwaa moja na wabunge wa Chadema kumnadi mgombea wa udiwani wa chama hicho wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche alisema katika mkutano huo watakuwepo wabunge wa chama hicho, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu (Mbeya Mjini) na Upendo Peneza ambaye ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Simiyu.

Alisema mkutano huo utakaofanyika leo katika mtaa wa Mkuyuni Kata ya Turwa mjini hapa, pia unatarajia kuwa wa kusisimua kwa wakazi wa mji wa Tarime na vitongoji vyake kutokana na ujio wa wana siasa hao machachari.

Itakuwa mara ya kwanza Sugu kuhutubia wilayani Tarime tangu achaguliwe ubunge pia itakuwa mara ya kwanza kwa Zito Kabwe ambaye hivi karibuni alitangaza kuwaunga mkono Chadema kufika katika kampeni hizo wilayani humo.

Katibu huyo wa Chadema Mkoa wa Mara alisema kuwa anatamani kuona kampeni zenye utulivu wa hali ya juu zikifanyika katika Kata ya Turwa na kuomba Jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu na badala yake kulinda hali ya amani katika uchaguzi huo.

Katika uchanguzi huo, CCM imemsimamisha Chacha Ghati (Chacha Kamanda) huku Chadema ikimsimamisha Charles Mnanka kuwania nafasi hiyo ya udiwani wa Kata ya Turwa kuziba pengo lililoachwa na Zakayo Wangwe aliyekuwa diwani kupitia Chadema baada ya kutimukia CCM kwa nia ya kuunga mkono juhudi za Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz