Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ziara ya kishindo ya Dk Bashiru Ally Zanzibar

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alifanya ziara ya siku nne Zanzibar yenye lengo la kujitambulisha pamoja na kuendeleza uhai wa chama, huku akiitumia kujibu tamko la Marekani kuhusu uchaguzi mdogo uliopita.

Kuna mengi ndani ya ziara hiyo, ambayo kwa njia moja au nyingine ni harakati za CCM kuibuka kivingine katika mwonekano miongoni mwa wanachama na wapinzani wao.

Mapokezi ya aina yake

Mbali na mapokezi ya aina yake baada ya kukanyaga visiwani na kulakiwa na viongozi mbalimbali wa CCM Zanzibar, Dk Bashiru aliandaliwa mapokezi mengine maalum kutoka Mnara wa kisonge hadi makao makuu ya CCM Zanzibar, Kisiwandui, yakiwashirikisha wanachama wa chama hicho kutoka mikoa mitatu ya Unguja, na baadaye akaelekea kisiwani Pemba.

Ayanyooshea vidole mataifa ya nje

Akihutubia katika viwanja vya Kisiwandui mjini Unguja, Dk Bashiru alianza na kuyaonya mataifa aliyosema yanaingilia mambo ya Tanzania, hasa katika masuala ya ndani, ambayo hayahitaji kuingiliwa.

Anayataka mataifa hayo yaache tabia ya kuingilia siasa za ndani ya Tanzania, badala yake yaangalie siasa za kwao na kuondosha migongano iliopo.

Anasema ni lazima nchi hizo hasa zenye Balozi Tanzania ziheshimu Katiba na miongozo ya kisheria ya nchi, vinginevyo Tanzania itashindwa kuvumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya balozi wanazowakilisha nchini.

Dk Bashiru anasisitiza kuwa Tanzania ni taifa huru linalojitawala na hakuna nchi yoyote itakayoweza kuiyumbisha demokrasia ya nchi hii.

Ingawa hakutaja nchi yoyote, anasema kumejitokeza baadhi ya mataifa yanayojifanya viranja wa demokrasia ambayo yamekuwa na tabia ya kutoa matamko ya kuhusu ushindi wa CCM wakati hazijasajiliwa kufanya kazi za kisiasa kama wanavyotoa vipeperushi vyao.

Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa katika siku za hivi karibuni kumetokea “taifa moja la kibeberu” linatuma matamko kwenye mitandao na kubeza ushindi wa CCM, hivyo ni vyema mataifa hayo yaheshimu utawala na demokrasia iliyoko nchini Tanzania. Alisema kuwa hakuna taifa lenye haki ya kubeza ushindi wa CCM inaoupata katika chaguzi ndogo zinazofanyika nchini, kwani kufanya hivyo ni kuingilia siasa za ndani za taifa hili.

Katika maelezo yake amebainisha kwamba kinachotakiwa kitambulike ni kuwa CCM haitishwi na matamko ya aina hiyo ya kuibeza na kuwataka wageni hao waache kuidharau Tanzania kwa kisingizio cha kutoa misaada.

“Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kweli kwa kupitia misingi ya Azimio la Arusha na mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, hivyo waache kuingilia shughuli za uendeshaji wa Tanzania,” anasema Dk Bashiru.

“Hatutishwi wa vipeperushi vinavyoitwa vipeperushi, na rafiki wa kweli ni yule anayebembeleza maelewano. Nchi yetu ni ndogo ila tunaendeleza mapambano, hatutwishi na watu na wala hatuwezi kuingiliwa,” anasema Dk Bashiru.

Dk Bashiru anabainisha kuwa licha kuwa Tanzania ni taifa maskini, serikali chini ya utawala wa CCM itajipanga katika kuimarisha uchumi pamoja na kulijenga taifa bila ya kutegemea msaada wa mtu yeyote ambaye atakuwa na masharti magumu.

Ingawa hakutaja taifa lolote, Marekani kupitia ubalozi wake nchini ndiyo ilitoa tamko la kukemea masuala mbalimbali yanayojitokeza katika chaguzi ndogo zinazoendelea;

Awasuta wanaosaka urais wa Zanzibar

Akizungumzia kuhusu makada walioanza kusaka urais visiwani Zanzibar kurithi kiti cha Dk Ali Mohamed Shein, Dk Bashiru ametumia ziara hiyo kutoa onyo kali akisema muda wa kufanya hivyo haujafika.

Dk Bashiru anaweka bayana kuwa wapo baadhi ya wanaCCM wameanza kuandaa makundi maalumu ya kupanga mikakati kuwania nafasi ya urais, kitendo ambacho ni kinyume na katiba ya CCM.

Anasema baadhi yao wanatambulika, wamekuwa wakifanya vikao vya siri katika maeneo mbalimbali eti kuandaa mipango ya kumrithi Dk Shein mwaka 2020.

“Baadhi ya watu hao hata sifa ya kuwa wakuu wa wilaya hawana,” anasema.

Katibu mkuu huyo anaweka bayana kuwa chama kitawachukulia hatua wote watakaobainika kuwamo katika kundi la kusaka urasi wa Zanzibar kinyume na taratibu.

“Kwanza niwaambie wakome kabisa kufanya hivyo, lakini pia wajiandae kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu bila ya kumuonea aibu mtu yeyote,” anaonya msomi huyo wa masuala ya siasa.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, kiongozi mzuri ni yule anayeombwa agombanie, si yule mwenye kuonesha uchu wa madaraka kwa kuanza kusaka nafasi ya uongozi kwa nguvu zake zote.

Anasema CCM hivi sasa haiihitaji viongozi wenye uchu, akidai viongozi wa aina hiyo ndio waliochangia kuondosha imani kwa wananchi kipindi cha nyuma.

“Niwaombe sana mumwachie Dk Shein amalize uongozi wake bila ya kubughudhiwa na makundi ya wasaka urais,” anasema Dk Bashiru.

Mali za CCM

Akiwa katika ziara yake hiyo visiwani hapa Dk Bashiru aliyeongoza timu ya kuhakiki mali za chame, anasema CCM imeamua kudhibiti mianya ya ubadhilifu wa rasilimali fedha na mali zake ili iweze kujitegemea kiuchumi na kuachana na dhana ya utegemezi.

Alisema endapo rasilimali hizo zitatumika vizuri na kuanzishwa kwa miradi mingine mikubwa ya uzalishaji wa kipato katika ngazi mbalimbali za chama na jumuiya zitawanufaisha wanachama wote badala ya watu wachache.

Dk Bashiru anasema lengo la kusimamia dhana ya ukuaji wa uchumi ndani ya chama kupitia vyanzo vyake vya mali na fedha, ni kukiondosha chama katika mazoea ya kutegemea ufadhili wa watu wenye fedha wanaokuwa na malengo ya kujinufaisha wenyewe kisiasa.

Pia, aliyataja malengo mengine kuwa ni uimarishaji wa maslahi ya watumishi wa CCM na jumuiya zake kwani bado maslahi yao ni ya kiwango cha chini ambayo hayaendani na hadhi ya taasisi yenyewe.

“Kwa miaka mingi chama chetu kimeondoka katika misingi ya kujitegemea badala yake kujitokeza kwa watu wenye fedha kukichangia chama wakati wa uchaguzi na shughuli nyingine za kitaasisi, sasa katika mageuzi haya ya kimuundo tuna dhamira ya chama chetu kukiondosha huko na tukaweza kutumia mali zetu wenyewe kujiendesha kitaasisi,” anasema Dk Bashiru.

Malengo hayo yakifanikiwa, Dk Bashiru anasema utakuwa ni ushindi mkubwa kwa wanachama wa CCM wote kwani tabia za rushwa na makundi ya kusaka nafasi za uongozi kwa kutumia fedha yatakuwa yamedhibitiwa.

Anawataka viongozi wote wa taasisi hiyo kuunga mkono malengo hayo kwa kuhakikisha wanapunguza matumizi holela ya fedha na badala yake waanzishe miradi itakayowasaidia kujiendesha ili kulinda heshima na hadhi ya CCM mbele ya jamii.

Pamoja na hayo, anazitaka jumuiya zote hasa ya umoja wa vijana (UVCCM) kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa kutumia rasilimali walizonazo kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo, uvuvi na viwanda vidogovidogo ili vijana wajiajiri wenyewe.

Pamoja na hayo yote, jambo moja kubwa linabaki kinywani mwa Dk Bashiru, kuwa wale wote waliohusika na kutapeli na kujimilikisha mali za taasisi hiyo kinyume na utaratibu, watachukuliwa hatua za kisheria.

Awaita wapinzani CCM

Kuhusu vyama vya upinzani Zanzibar, Katibu mkuu wa CCM anavitaka kuendelea kujiunga na CCM kwa kuwa chama cha CUF hakina tena mvuto kwa jamii kutokana na alichoita tabia ya unafiki na uongo inayofanywa na viongozi wakuu wa chama hicho.

“Wanachama wa vyama vya upinzani njoo CCM, huku tupo shwari na tumekamilika kila idara. Wala msihofu chochote, hakuna mtu yeyote wa kuwagusa, na wale wote waliojiunga na chama chetu leo nawahakikishieni kuwa mtafaidika na siasa safi na demokrasia iliyotukuka.

“Wana CCM wenzangu, hawa wenzetu wanaojiunga na CCM (wanachama 92) wapokeeni na tuwathamini kwani wamefanya maamuzi sahihi ambayo hawatoweza kuyajutia wawapo hapa,” anasema Dk Bashiru.

Alisema lengo la CCM hivi sasa ni kuhakikisha inaendelea kuvunja ngome zote za upinzani kabla ya mwaka 2020, hiyo ni kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Dk Bashiru anaongeza kuwa CCM ipo imara na itapata ushindi wa kihistoria mwaka 2020 kwa nchini nzima, kuliko ushindi unaopatikana sasa katika uchaguzi mdogo unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia sababu za kushinda, Dk Bashiru anasema vyama vya upinzani vimekosa mwelekeo na ndio maana wanachama wake wanahamia CCM kwa wingi.

Dk Bashiru anasema kila mwana CCM anatakiwa kulinda Muungano, mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa ni tunu na chimbuko la mafanikio yaliyopo hivi sasa na bila kuyalinda hakuna maendeleo yatakayopatikana visiwani.

Azungumza na Dk Shein, Seif

Katika ziara hiyo, Dk Bashiru alipata nafasi ya kuzungumza na Makamo mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk Shein pamoja na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akieleza jinsi chama hicho kilivyojipanga na kitakavyochukua hatua za kukabiliana na makundi ndani yake yenye kukiathiri na kukidhoofisha.

Alisema katika mwelekeo wa uendelezaji wa CCM imara iliyoanza kurejesha imani kwa wananchi walio wengi, suala la makundi limefikia kikomo.

“Katika utumishi wangu wa chama katika nafasi ya utendaji mkuu sitokubali kuchafuka wala kuchafuliwa, wala kuwachafua viongozi wetu wakuu walioniamini kunipa utumishi huu muhimu katika chama,” anasisitiza.

Kauli za viongozi

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Saadalla anamweleza karibu mkuu kuwa chama hicho visiwani kimejipanga vizuri na wanachama katika ngazi zote, na tayari wameshashuka nyumba kwa nyumba kujua changamoto zinazowakabili wananchi ili zifanyiwe kazi kwa vitendo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib anasema hali ya kisiasa katika mkoa huo ipo shwari na CCM imeendelea kuimarika huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba , Yussuf Ali Juma akisema wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha CCM inashinda kwa ngazi zote katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Chanzo: mwananchi.co.tz