Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema Jimbo la Kawe Dar es Salaam kimepata pigo baada ya Diwani wake wa viti maalum, Carolina Kazinza na Katibu wa jimbo hilo, Andrew Samsoni kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wanachama hao wamejiunga na chama hicho leo Jumapili Septemba 1, 2019 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ya kukagua uhai wa chama sambamba na ufunguzi wa mashina katika majimbo ya Jiji la Dar es Salaam.
Wengine waliojiunga na CCM ni pamoja na aliyekuwa Diwani wa Makongo, Deusdedit Mtilo na mwanasheria wa kanda ya Pwani wa Chadema, Nadia Karama.
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani, Andrew amesema hawezi kuwa mnafiki kutokana na kazi zinazifanywa na Rais John Magufuli wa Tanzania.
Amesema yenye ndiye aliyeleta madiwani na mbunge wa jimbo la kawe (Halima Mdee-Chadema) hivyo ameamua kurudi mwenyewe kwa maslahi ya Taifa.
"Mimi ndiye niliyemchukulia Mdee fomu ya ubunge, nimerudi mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yoyote kutokana na kazi anazozifanya Mheshimiwa Rais," amesema Samson