Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ZEC: Msihofu kura ya mapema

75ce8fd882306e5f2b4f973c70962814 ZEC: Msihofu kura ya mapema

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Huduma za Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Idrissa Jecha amewataka wananchi na viongozi wengine wa vyama vya siasa kuondoa wasiwasi kuhusu kura ya mapema visiwani Zanzibar.

Alisema lengo kubwa ni kutoa fursa kwa watendaji wenye majukumu muhimu ikiwemo ya ulinzi katika siku ya uchaguzi mkuu kutumia haki yao kupiga kura.

Akizungumza na gazeti hili Jecha aliwataja watu watakaohusika kupiga kura ya mapema katika siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 ni wapiganaji wa vyombo vya ulinzi ikiwemo askari wa Jeshi la Polisi ambao watakuwa na majukumu ya kusimamia shughuli za uchaguzi mkuu.

Alisema kura hiyo inafanyika baada ya sheria ya uchaguzi nambar 11 ya mwaka 1984 kufanyiwa marekebisho na Baraza la Wawakilishi na kupitishwa kwa sheria namba 4 ya mwaka 2018.

''Kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 ambayo imetajwa katika sheria hiyo kuwaruhusu wasimamizi wa ulinzi na watendaji wa Tume ya uchaguzi kutumiya haki ya kidemokrasia kupiga kura kwa mujibu wa sheria''alisema.

Aliwatoa hofu wananchi na wanasiasa kwamba kura hiyo itafanyika kwa uwazi na demokrasia na hakuna mbinu wala ghilba zitakazofanyika.

Alisema utaratibu wa kura ya mapema umekuwa ukitumika katika nchi mbali mbali ikiwemo Marekani ambao hutowa fursa kwa watendaji wa vyombo vya ulinzi na wafanyakazi wa Tume ya uchaguzi (ZEC) ambao katika siku ya uchaguzi watakuwa wanaratibu zoezi hilo.

Kwa mfano alisema kwa upande wa Zanzibar katika miaka mingi wafanyakazi wa vyombo vya ulinzi ikiwemo Jeshi la Polisi wanaosimamia amani na watendaji wengine wa Tume ya uchaguzi hawapati nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo kwa njia ya kuchaguwa viongozi wao kutokana na kutingwa na majukumu.

''Hizo ndiyo sababa zilizopelekea kuwepo kwa kura ya mapema...ipo kwa mujibu wa sheria na malengo yake makubwa kutoa nafasi kwa watendaji ikiwemo wa vyombo vya ulinzi watakaoshughulikia harakati za uchaguzi kupiga kura mapema''alisema.

Mapema Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Faina Idarous amesema Uchaguzi Mkuu utafanyika katika mazingira ya amani na demokrasia na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi ambao watakuwa tayari kuwaletea maendeleo.

Aidha aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kukamilisha mchakato wa Demokrasia huku matarajio makubwa ya kuwepo kwa amani na utulivu.

''Hayo ndiyo matarajio ya Tume ya uchaguzi ya Zanzibar....kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi na kupiga kura kwa amani ili kupata viongozi watakaoleta maendeleo''alisema.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa akiwemo mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo maalim Seif Sharif Hamad amekuwa akihoji kuwepo kwa kura ya mapema ambayo imepitishwa kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: habarileo.co.tz