Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yusuf Makamba asubiria kwa hamu kuitwa CCM

91972 Makamba+pic Yusuf Makamba asubiria kwa hamu kuitwa CCM

Thu, 16 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Ikiwa zimetimia siku 34 tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka waliokuwa viongozi wake kwa nafasi mbalimbali ikiwamo makatibu wakuu wawili wa zamani kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho, ukimya umetawala juu ya kile kinachoendelea.

Desemba 13 mwaka jana, Halmashauri Kuu ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli iliyokutana jijini Mwanza iliwasamehe baadhi ya wanachama waliokuwa na makosa lakini ilitoa agizo kwa kamati hiyo kuwaita makada wake watatu.

Wanaopaswa kuhojiwa na kamati hiyo ni; Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana ambao waliwahi kuwa makatibu wakuu wa CCM kwa nyakati tofauti pamoja na aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu, Bernard Membe.

Tangu kutolewa kwa azimio hilo, ukimya umetawala na hakuna taarifa kutoka ndani ya CCM zinazozungumzia suala hilo hali iliyolifanya Mwananchi kuwatafuta walengwa ili kujua hasa kipi kinaendelea au kama kuna barua ya wito imekwisha kutumwa kwao.

Miongoni mwa waliozungumza na Mwananchi ni Makamba ambaye alisema hadi sasa hajapata wito wa kuhudhuria wa Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho na kwamba akiitwa hatochelewa kwenda. “Akuitaye kajaza, ukichelewa atapunguza.” Ndivyo alivyosema Makamba huku akifafanua kuwa mtu anayekuita ukichelewa kwenda kama ana mambo 10 atazungumza matano, mengine atasema yamepitwa na wakati.

Alisema mtu anapokuita ili akueleze mambo yote ni vema ukawahi kufika hivyo yeye hatochelewa kuitikia wito.

“Katika jambo nalisubiri kwa hamu ni hilo, hata ikiwa Mwanza nitakwenda. Sitachelewa kwenda,” alisema Makamba ambaye amewahi kushika nafasi kadhaa za uongozi ndani ya Serikali na CCM.

Hata hivyo, Makamba ambaye pia amewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alisema hana hofu ya kuitwa kwenye kamati hiyo ndio maana anausubiri wito huo kwa hamu.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alipotafutwa jana kuhusu ratiba ya kuwahoji makada hao, simu yake iliita bila majibu na alipotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz