Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

YALIYOTIKISA 2019: Lowassa atangaza kurejea CCM, ndege ya Ethiopia yaua 157

90076 Matukio+pic YALIYOTIKISA 2019: Lowassa atangaza kurejea CCM, ndege ya Ethiopia yaua 157

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mwaka 2015 alitikisa anga za siasa alipokuwa waziri mkuu wa kwanza kuhama CCM na kujiunga na upinzani, hali ilikuwa tofauti mwezi Machi mwaka huu wakati Edward Lowassa alipotangaza kurejea chama hicho.

Siku hiyo, Machi mosi, alikuwa kwenye gari moja na Rostam Aziz wakitokea ofisi zake kwenda ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. Rostam alikuwa akiendesha gari hilo na walipofika Lumumba alikuta mwenyekiti wa CCM, John Magufuli na viongozi wajuu wakiwasubiri nje ya jengo ambalo liko pembeni ya barabara.

A|lishuka na kusalimiana na viongozi hao na baadaye kusema kwa kifupi kuwa ameamua “kurejea nyumbani”.

Akiwa na nia ya kuendeleza “safari ya matumaini” iliyoonekana imekatishwa na CCM baada ya jina lake kuenguliwa miongoni mwa makada waliokuwa wanataka wapitishwe na chama hicho kugombea urais, Lowassa alijiunga na Chadema Julai 28 na baada ya vikao vingi vya viongozi wa juu, alipitishwa kugombea urais na chama hicho kikuu cha upinzani.

Na hiyo ilimaanisha kuwa ndiye aliyepewa jukumu la kugombea urais na vyama vingine vitatu vya upinzani vya NCCR-Mageuzi, NLD na CUF vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Na kishindo chake kilikuwa dhahiri. Alipata kura milioni 6.07 na kuwa mgombea pekee wa upinzani aliyewahi kupata kura nyingi.

Lakini akadumu Chadema kwa muda wa siku 1,312 kabla ya kuamua kutangaza “kurudi nyumbani”.

Lowassa amekuwa mwanachama wa CCM kwa muda mrefu na alijaribu mara mbili kugombea urais 1995 na 2015 kupitia chama hicho lakini hakupitishwa.

Hata kabla ya kurejea CCM, tetesi zilishaanza muda mrefu, lakini Novemba 17, 2017 akiwa jijini Arusha alikanusha tetesi hizo.

“Huu ni uongo wa kutunga. Wamekuwa wakitunga vitu vingi juu yangu. Mimi sina mpango wa kurejea CCM,” Lowassa aliiambia Mwananchi wakati huo.

Pamoja na ubashiri kuwa mkubwa, kurejea kwake CCM kulionekana kwa ghafla na tangu wakati huo haonekani mara kwa mara hadharani wala kuzungumzia masuala ya kisiasa.

Ajali ya Ethiopian Airlines

Tukio jingine lililotokea Machi lilikuwa ni ajali ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 ambayo ilianguka Machi 10 muda mfupi baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole uliopo, Addis Ababa, Ethipia na kusababisha vifo vya watu 157 wakiwamo abiria 149 na wafanyakazi wanane.

Ndege hiyo ambayo ni ya shirika la Ethiopia ilikuwa ikielekea Nairobi, Kenya lakini muda mfupi baada ya kuruka ilipoteza mawasiliano na rada. Ilibainika baadaye kuwa ilikuwa na hitilafu katika mfumo wake wa kompyuta ambao hulazimisha ndege kutua chini kunapokuwa na tatizo, lakini mfumo huo haujaeleweka vizuri kwa marubani.

Hiyo ilikuwa ni kashfa iliyosambaa duniani kote kwa haraka hasa baada ya kubainika kuwa tatizo hilo pia lilisababisha ndege ya Indonesia kuanguka mwaka jana.

Kutokana na tatizo hilo, iliagizwa ndege hizo zisifanye safari hadi tatizo litakapopatiwa ufumbuzi na hivyo mashirika ya usafiri wa anga yakaamua kusimamisha matumizi ya ndege hizo na hadi sasa hakuna ufumbuzi.

Ufungaji wa maduka ya fedha

Tukio jingine lililotikisa mwezi Machi ni kitendo cha Benki Kuu (BOT) kufanya ukaguzi katika maduka ya kubadilishia fedha na baadaye kuyafunga kutokana na kukiuka sheria. Mpango huo ulianzia mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na baadaye Dar es Salaam.

BOT ilielekeza kwamba huduma ya kubadilisha fedha zitaendelea kutolewa katika benki zote hapa nchini. Ukaguzi huo wa BOT ilibaini kwamba maduka mengi ya fedha yanafanya biashara hiyo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu hivyo, walianzisha utaratibu wa kufuta leseni za maduka yanayokiuka masharti ya biashara hiyo.

Mwalimu ahukumiwa kifo

Jaji wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha alitumia hoja 12 kujibu swali la mwalimu Respicius Mutazangira (51) aliyemuua mwanafunzi Sperius Eradius (13) wa Shule ya Msingi Kibeta na kumhukumu kunyongwa hadi kufa huku akimwachia huru mwalimu mwenzake Heriet Gerald (47).

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 6 na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba huku ikishuhudiwa na umati wa watu uliokuwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya kesi hiyo.

Jaji Mlacha alilazimika kutumia kipaza sauti kusoma hukumu hiyo ili kila aliyekuwa eneo la Mahakama asikie alichokuwa akisema.

Mbowe, Matiko waachiwa

Machi 7, Mahakama Kuu iliwaachia huru, mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambao walikaa mahabusu Segerea kwa siku 104.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Jaji Sam Rumanyika kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu wa kuwafutia dhamana wawili hao kwa kosa la kukiuka masharti waliyopewa.

Alisema kabla ya mahakama kumfutia mshtakiwa dhamana lazima kwanza mdhamini apewe nafasi ya kujieleza kuhusu kutwaliwa kwa fungu lake na iwapo mshtakiwa ataendelea kutoonekana ndipo litwaliwe na iwapo hataonekana, ndipo dhamana ifutwe.

Lipumba achaguliwa CUF

Machi 13, Mkutano Mkuu wa CUF ulimchagua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho, huku katiba ya chama hicho ikifanyiwa mabadiliko na kumpa nguvu ya kuteua majina matatu ya makatibu wakuu akishauriana na viongozi wenzake kabla ya kuidhinishwa na mkutano mkuu.

Muda mfupi baada ya kuteuliwa, Profesa Lipumba alimteua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa Katibu Mkuu wa CUF, akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa akishika nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Itakumbukwa, Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF mwaka 2015 kwa madai kwamba hakuridhishwa na uamuzi wa viongozi wa Ukawa kumpitisha Lowassa kama mgombea wao wa urais.

Maalim Seif ahamia ACT Wazalendo

Machi 19, Maalim Seif Sharif Hamad, mwamba wa siasa za Zanzibar, alianza safari mpya ya kisiasa ndani ya chama cha ACT Wazalendo, akikabidhiwa kadi namba moja.

Maalim Seif alichukua uamuzi huo baada ya mvutano na Profesa Lipumba ambao ulianza baada ya Profesa Lipumba kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo.

Maalim Seif alihama CUF baada ya kushindwa katika kesi iliyofunguliwa kuomba mwongozo wa mahakama.

Nassari avuliwa ubunge

Machi 14, Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alipoteza sifa ya kuendelea na ubunge baada ya kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo ya Bunge.

Taarifa iliyotolewa jana na Bunge, ilitaja mikutano hiyo kuwa ni wa 12 ulioanza Septemba 4 hadi 14 na Novemba 6 hadi 16, 2018 pamoja na ule wa Januari 29 hadi 9, 2019.

Taarifa iliyotolewa na Bunge ilisema Spika Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu kuwa jimbo hilo lipo wazi kutokana na mbunge wake kupoteza sifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz