Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wingu zito Nassari kuvuliwa ubunge

47112 Pic+wingu

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arumeru, Wingu zito limetawala tukio la kung’olewa ubunge mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari huku wananchi, viongozi wa Chadema na wale wa kimila wakionekana kuwa na mitazamo tofauti.

Hata hivyo, wingu hilo huenda likapata mwangaza leo ambako Nassari anatarajiwa kuweka wazi nini kimemtokea hadi kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Alhamisi iliyopita, Spika Job Ndugai aliiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) barua akiieleza kuwa Nassari amepoteza sifa ya kuwa mbunge baada ya kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo bila kutoa taarifa.

Katika mkutano wake uliopangwa kufanyika leo katika makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Nassari anatarajiwa kuelezea mwanzo-mwisho wa kilichotokea ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Freeman Mbowe.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, akizungumza juzi na waandishi alisema amemwagiza Nassari kuzungumza kinaga ubaga kipi kimetokea hadi akavuliwa ubunge.

Tangu kutoka kwa agizo hilo, Nassari ameahirisha mkutano huo mara tatu. Juzi, alipanga kuzungumza saa nane mchana akiwa Arusha akaahirisha, na kupanga kufanya hivyo jana lakini aliahirisha tena hadi leo.

Mwananchi lilipotaka kujua sababu za kuahirisha alisema mazingira ya Arusha si rafiki kulinganisha na Dar es Salaam ndiyo sababu ya kuamua kuja kuzungumzia jijini humo. Kuhusu juzi, alisema asingeweza zungumza wakati Mbowe amezungumza.

Akizungumzia kitendo cha mbunge huyo kuvuliwa wadhifa wake, mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Arumeru Mashariki, Gadiel Mwanda alisema majibu mengi anaweza kuyatoa Nassari mwenyewe.

Kaimu katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure alisema chama hicho, kinafuatilia kwa kina sakata la Nassari na hadi sasa hakiamini kama amenunuliwa au amefanya njama za kuuza jimbo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa mila wamemtupia Lawama Nassari kwa kilichotokea na wamepongeza Spika Ndugai.

Kiongozi mkuu wa mila ya Kimeru maarufu kama mshiri mkuu, Hezron Sumari alisema kitendo alichofanya Nassari ni kuwadharau wananchi waliomchagua na kumpongeza Spika kwa hatua aliyoichukua.

Hata hivyo, mshiri mwingine, Emmanuel Urio alisema anaamini Nassari ana sababu za kwa nini hakuingia bungeni na kuwalaumu viongozi wenzake wa mila kuanza kufanya siasa, “wametoa tamko viongozi wenzangu lakini sisi kama Washiri hatupaswi kufuata vyama. Hawa wenzangu wanafanya siasa.”

Wakazi wa Arumeru, Kanangira Michael na Elirehema Nnko, walitaka majibu ya kina kwa pande zote yatolewe kuhusiana na tukio hilo.

Kanangira alisema, “kuna maneno kuwa mbunge wetu ameuza jimbo, wengine wanasema anataka kujiunga na CCM, sasa lazima ajibu mwenyewe tujue ukweli.”

Hata hivyo jana Mwananchi lilipomuuliza Nassari kuhusu hoja hiyo alisema, “Huwezi kuzuia watu kufikiri.”

Soma zaidi: Mwenyekiti Meru amtetea Joshua Nassari



Chanzo: mwananchi.co.tz