Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri atoa Sh1.2 bilioni kutatua shida ya maji Jimbo la Monduli

16712 WAZIRI+PIC%255C TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesema Serikali imetoa kiasi cha Sh1.2 bilioni kutatua tatizo la maji katika mji wa Monduli na kuwataka wananchi kumchagua Julius Kalanga wa CCM ili aweze kuzisimamia.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika uwanja wa Monduli mjini, Aweso alisema Serikali inatambua kero za wananchi wa Monduli na tayari ilianza kuzifanyia kazi.

Aweso alisema kazi ya mbunge ni kuwatetea wananchi na Kalanga alikwisha anza kazi hiyo na ndio sababu Serikali ilitoa fedha kwa wilaya hiyo lakini alikuwa anakosa ushirikiano na sasa ataupata baada ya kujiunga na CCM.

Hata hivyo, Aweso alionya mtu yoyote mwenye mpango wa kula fedha hizo atazitapika mapema.

“ Mimi ni mdogo lakini najiamini, ukizingua tunazinguana nakutimua..Sitakubali kutumbuliwa na Rais John Magufuli watu wakikosa maji,”alisisitiza.

Akizungumza katika mkutano huo, Kalanga aliishukuru Serikali kwa kutambua kero za wananchi wa Monduli na kuanza kuzifanyia kazi.

Hata hivyo, Kalanga aliomba Serikali kutazama upya gharama za kuunganisha maji na badala yake ipunguwe kwani Sh400,000 ni kubwa sana.

“Wananchi wangu wanashida ya maji, lakini gharama ni kubwa tunaomba naibu waziri utusaidie hili lakini pia kuna gharama za kuchimba msingi tunaomba kama wananchi wanaweza wafanye wao,” aliongeza.

Meneja kampeni wa CCM Monduli, William Ole Nasha alisema chama hicho kitaendelea kupokea kero za wananchi na kufanyiwa kazi.

“Niliahidi kuwaleta mawaziri mbalimbali wamekuja na wamesikiliza kero.”

Kwa mujibu wa meneja huyo tangu kuja kwa mawaziri hao kero ambazo zinaweza kutatuliwa zimetatuliwa.

“Kikubwa tunawaomba kumchagua Kalanga ili asimamie ahadi hizi,” alisema meneja huyo.

Nasha aliongeza pia kuwa katika wilaya hiyo alibaini kero ya shule kutosajiliwa licha ya wananchi kuzijenga lakini sasa shule zote zimesajiliwa na tatizo hilo kuisha.

Alisema wananchi wasiwe na wasiwasi na Kalanga kwani amekuja kuwaletea maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz