Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Jafo amaliza mchezo

85960 Pic+jafo Waziri Jafo amaliza mchezo

Wed, 27 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati CCM ikizoa ushindi mitaa yote 4,263 nchini, vyama sita vya siasa vimetajwa kupata nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Vyama sita kati ya 19 vilivyopata nafasi za uongozi ni CCM, Chadema, CUF, ACT Wazalendo, UDP na DP.

Hata hivyo, vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na CUF vimetajwa kupata viti wakati vilitangaza kujitoa mapema.

Akitangaza matokeo jana, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo alisema jumla ya wapiga kura milioni 19.6 walijitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi huo.

Alisema kati ya hao wanaume walikuwa ni milioni 9.5 na wanawake milioni 10.1, idadi ambayo ni sawa na asilimia 86 ya lengo la uandikishaji ambalo lilikuwa ni wapiga kura milioni 22.9.

Alisema katika shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu jumla ya watu 555,036 walifanikiwa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi mbalimbali.

Alisema watu 539, 993 sawa na asilimia 97.3 walifanikiwa kurejesha fomu zao.

Jafo alivitaja vyama 19 vilivyoshiriki katika hatua mbalimbali za uchaguzi huo kuwa ni CCM, Chadema, CUF na ACT- Wazalendo.

Vingine ni NCCR-Mageuzi, UPDP, NLD, NRA, SAU, ADA, ADA-TADEA, TLP, UDP, Demokrasia Makini, DP, AFP, CCK, ADC, UMD na Chauma.

Katika orodha ya Jafo vimo vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, ACT-Wazalendo, UPDP na Chauma ambavyo vilitangaza kujitoa mapema.

Vyama hivyo vilijitoa vikilalamikia kukiukwa kwa mchakato mzima kutokana na wagombea wao kuenguliwa au kunyimwa fomu.

Jafo alisema wagombea wa CCM katika mikoa minne walipita bila kupingwa kwenye uchaguzi huo ambayo ni Tanga, Katavi, Ruvuma na Njombe.

Alisema wagombea wa CCM waliopita bila kupingwa katika uchaguzi huo walikuwa 316, 474.

Alifafanua kuwa katika nafasi ya uenyekiti wagombea wa CCM waliopita bila kupingwa walikuwa ni katika vijiji 12028, vitongoji 62,927 na mitaa 4207.

Alisema katika kundi la wanawake waliopita bila kupingwa walikuwa ni 105,953 wakati kwenye kundi la mchanganyiko walikuwa ni 131, 359.

Alisema Chadema kilipita bila kupingwa katika nafasi 69 ambapo kati ya hizo kundi la wanawake zilikuwa 27 wakati kundi la mchanganyiko 42.

Kwa upande wa CUF, kilipita bila kupingwa katika nafasi nane huku kundi la wanawake wakiwa watatu na mchanganyiko watano.

Kwa upande wa ACT Wazalendo waliopita bila kupingwa walikuwa 12, mmoja alipita katika kundi la wanawake na wagombea 11 kwenye kundi la mchanganyiko.

Alisema katika uchaguzi huo kuna vyama vya siasa vilitangaza kujitoa lakini kwa mujibu wa kanuni alifafanua kuwa anayepaswa kujitoa ni mgombea mwenyewe ama ngazi iliyomdhamini.

Jafo alisema katika mchakato wa uchaguzi huo nafasi zilizokuwa zinawania ni 332,160. Katika nafasi hizi vijiji vilikuwa 12,262, mitaa 4,263, vitongoji 63,992, nafasi kundi la wanawake 106,622 na kundi mchanganyiko 145,021.

Jafo alisema CCM kilijizolea uenyekiti katika vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9 mitaa 4,263 (100%) na vitongoji 63, 970 (99.4%).

Katika kundi la wanawake wameshinda nafasi 106,577 sawa na asilimia 99.96 wakati kundi la mchanganyiko wamezoa nafasi 144,925 sawa na asilimia 99.9.

Alisema Chadema imeshinda uenyekiti wa vijiji nafasi moja, vitongoji 19 lakini haikupata mtaa hata mmoja.

Alisema katika kundi la wanawake, chama hicho kimeshinda nafasi 39 huku kundi la mchanganyiko wakipata nafasi 71.

Alisema kwa upande wa CUF waliambulia kijiji kimoja katika nafasi ya uenyekiti huku mitaa kikifanikiwa kupata miwili.

Alisema katika kundi la wanawake walishinda nafasi tatu huku katika kundi la mchanganyiko wakipata nafasi 14.

ACT Wazalendo kilipata uenyekiti katika kitongoji kimoja, kundi la wanawake nafasi moja na kundi la mchanganyiko nafasi 11.

Jafo alisema UDP walipata nafasi moja kwa wanawake huku chama cha DP kikiambulia nafasi moja kwa wanawake pia.

Chanzo: mwananchi.co.tz