Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazee wanavyotaka sera za wagombea 2020 kuwagusa

0f010a474e5c756a0aa487ef04d2f60c Wazee wanavyotaka sera za wagombea 2020 kuwagusa

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UPO usemi usemao kwamba wazee ni hazina. Busara na miongozo yao huziwezesha jamii kuishi maisha rafiki yasiyo na mitafaruku ya kudumu bali yenye kumalizika. Uwepo wao duniani kwa miaka mingi hufanya jamii inayowazunguka kuwatumia kama sehemu ya kujifunza uzoefu na ujuzi wao sambamba na kufahamu historia yao.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2013, mzee ni mtu yeyote aliye na umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea. Uzee na kuzeeka ni mchakato wa makuzi ya mwanadamu kuanzia utoto hadi uzee.

Kwa maana hiyo binadamu yeyote aliyezaliwa ni mzee mtarajiwa kwa kuwa anaweza tu kuukwepa uzee iwapo atakutwa na umauti kabla ya kufikia umri wa miaka 60.

Makala haya yanaangalia mambo ambayo wazee nchini wanatarajia kuona wagombea mbalimbali wakiyazungumzia kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ambazo zilianza rasmi wiki uliopita na zinatazamiwa kuhitimishwa Oktoba mwaka huu.

Hawa tunaowachagua ni viongozi watunga sera na sheria mbalimbali za nchi ikiwa ni pamoja na miongozo inayohusu maisha ya wazee na jamii zinazowazunguka.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na wazee wapatao milioni 2.5, sawa na asilimia 5.6 ya watanzania wote. Kati ya hao wazee wanawake walikuwa 1,307,358.

Kufikia mwaka 2050 Tanzania inakadiriwa kwamba itakuwa na wazee milioni 8.3, sawa na asilimia 10 ya watanzania wote. Hii ina maana kuwa wazee watakuwa wengi zaidi kuliko watoto wa umri wa miaka 14 kushuka chini.

Hata hivyo, wazee wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali. Kati ya hizo ni pamoja na kulazimika kulea watoto yatima ambao ni wajukuu zao.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya yatima na watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi Tanzania wanatunzwa na wazee.

Changamoto nyingine ni magonjwa na uangalizi madhubuti. Afisa miradi wa Shirika lisilo la kiserikali la KIWWAUTA linalojishughulisha na ufuatiliaji wa masuala ya wazee Tanzania bara, Moses Nchimbi, anasema karibu asilimia 60 ya vifo vya wazee vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kisukari.

Anasema theluthi moja ya wazee, kwa mujibu wa takwimu hizo wana ulemavu ama wa kuzaliwa nao au wameupata ukubwani.

Wazee wanasema unafuu wa changamoto zinazowakabili unaweza kupatikana endapo vyombo vya maamuzi vitajikita katika kuyapa kipaumbelea maoni na mapendekezo yanayotolewa na wazee wenyewe.

Kwamba uchaguzi huu uwe sehemu ya kuwanasua wazee kutoka kwenye dimbwi la maisha yasiyokuwa na uhakika wa kesho. Uwe sababu ya kuwafanya waishi kama ilivyo kwa watu wa umri mwingine.

Wazee wanataka kusikia wagombea wanasema nini kuhusu namna watakavyosimamia upatikanaji wa haki za wazee katika nyanja za kiuchumi, usalama na afya.

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wanaojihusisha na wazee mkoani Mbeya ulioandaliwa na Kiwwauta, wazee hao wanasema pamoja na Serikali kuwa na sera ya matibabu bure kwa wazee bado zipo changamoto katika upatikanaji wa huduma kwenye vituo vya matibabu.

Mmoja wa wazee hao, Raphael Ilomo, kutoka wilayani Chunya, anawataka watoa huduma za afya katika madirisha ya wazee wawe wale walio na moyo wa huruma na upendo wenye kutumia muda wao mwingi kuwasikiliza wazee na kuwaelewa kwa taratibu tofauti na watu warika jingine.

Anasema wazee kwa kawaida hawana utofauti na watoto hivyo wanahitaji lugha laini wanapoelezea matatizo yao na kusikilizwa na mtu asiye na uharaka.

“Haya yote yanawezekana iwapo watunga sera na vyombo vinavyosimamia sheria vitawashirikisha kwa karibu wazee na kutambua mahitaji yao,” anasema.

Anataka pia wagombea waeleze ni kwa namna gani watasimamia suala la upatikanaji wa uhakika wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwapunguzia wazee adha ya kurudi mara mbilimbili kufuata dawa pale wanapozikosa huku pia akishauri kuwepo kwa mawasiliano baina ya madirisha yanayowapa huduma na yale ya kutolea dawa.

Kwa upande wake, Mzee Edson Mwaibanje anawataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuwasiliana na wazee wa mila na viongozi wa kidini ili kutambua changamoto zinazowakabili wazee ili watakapochaguliwa waende kuzifanyia kazi badala ya kuzifanyia zile watakazozikuta kwenye makabrasha pekee maofisini.

Anafafanua kwamba hizo changamoto za kwenye makabrasha zinaweza zikawa zimeandaliwa na watu wasiozingatia matakwa halisi ya wazee.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa wa Mbeya, Hezron Kapwela anazitaja ajenda zinazopaswa kuelekezwa kwa wazee katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni pamoja na upatikanaji wa pensheni kwa jamii kwa wazee wakiwemo wale ambao hawakupata bahati ya kufanya kazi serikalini pamoja na urahisi wa upatikanaji wa huduma za afya.

Ajenda nyingine anasema ni kukomesha ukatili na mauaji dhidi ya wazee ambayo bado hayajakoma kabisa pamoja na wazee kuwezeshwa kiuchumi na jamii kupewa elimu ya maandalizi ya uzee na kuzeeka.

“Ajenda hizi ziliwahi kujadiliwa na utekelezaji wake utaleta mabadiliko makubwa kwa wazee na jamii kwa ujumla. Hizi zikifanyiwa kazi haitokuwa faida kwa wazee waliopo hivi sasa pekee bali na watu wazima wa leo wanaoelekea uzeeni.

“Tunazo ajenda pia za kukamilisha uundaji wa mabaraza ya wazee katika ngazi zote nchini yaani vijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa. Tunataka pia sera ya wazee ifanyiwe marekebisho na kutungiwa sheria. Tunataka kuwe na uwakilishi wa wazee katika vyombo vya maamuzi likiwemo Bunge kama tunavyoona kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu,” anasema Kapwela.

Anasema mazingatio ya ajenda hizi yanawezekana iwapo ‘ukondoishwaji’ wa masuala ya wazee utafanyika katika mipango na shughuli za kiuchumi na maendeleo. Na ili ukondoishwaji huo ufanyike ni lazima wagombea katika chaguzi mbalimbali wakajikita katika kutambua kada ya maze na mahitaji yao.

“Ukondoishwaji ni mkakati wa kuwezesha masuala muhimu yanayogusa maisha ya wazee na uzoefu wao kuwa sehemu muhimu ya mipango, ubunifu, utekelezaji, tathmini na ufuatiliaji sera na mipango na masuala ya jamii ili kuwawezesha wazee kunufaika kwa usawa bila ubaguzi,” anasema Makamu Mwenyekiti huyo.

Afisa ufuatiliaji wa Kiwwauta, Mussa Mcharo, anasema ukondoishwaji wa masuala ya wazee ni jukumu la kila mmoja katika halmashauri yaani watendaji na watawala wote wakiwemo mstahiki meya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara, wataalamu, watendaji wasaidizi katika idara/taasisi na halmashauri kwa ujumla.

“Wadau wa maendeleo pia ni muhimu kuzingatiwa. Hawa ni pamoja na viongozi wa kisiasa kama wakuu wa wilaya, wabunge na madiwani. Zipo pia asasi za kiraia, taasisi za kisheria, wafanyabiashara, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na Bima ya Taifa ya Afya (NHIF),” anasema Mcharo.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Mwanaidi Nyaruko, anasema kutokana na kundi la wazee kujikuta likilea yatima ni muhimu jamii zinazowazunguka kuzingatia mpango wa Bima ya Afya ya Jamii ili kuwapunguzia mzigo wa matibabu wa wanaowategemea licha ya wao kuwa kwenye mpango wa matibabu bure.

Anasema ni muhimu vyombo vinavyotunga sera na sheria kulitazama kundi hili na kutetea maslahi yake.

Dk Osimunda Mwanyika, Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Mbeya anaitaka jamii nchini kutambua kuwa jukumu ya kuwawekea mazingira mazuri ya kimaisha wazee ni ya kila mmoja badala ya kuiachia serikali pekee kutekeleza jukumu hilo.

Akimwakilisha mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya, Dk Mwanyika anasema kumekuwa na dhana ndani ya jamii ya kuilaumu na kuitaka serikali kutekeleza mambo mbalimbali kwa wazee lakini baadhi ya watu wanajisahau kuwa jukumu hilo linapaswa kuwa la pamoja kati ya serikali na wadau mbalimba ikiwemo jamii inayowazunguka wazee.

Anasema ni wakati sasa kwa wadau wote kuungana kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wazee nchini ili kuwawezesha kuishi maisha ya furaha na yenye kuwafanya kufarijika kwa kuishi na jamii inayowajali.

Anazitaja taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini kuona umuhimu mkubwa katika kuibua na kuhimiza jamii kuwa na mikakati ya kuwasaidia wazee ikiwemo kuhimiza uwepo wa mifuko ya wazee.

Anawahimiza wanasiasa wasibakie nyuma katika kuyaangazia maisha ya wazee na kwamba wasisahau kuwa na wao wanaelekea uzeeni.

Dk Mwanyika anapongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali nchini ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa matibabu, hatua anayosema imeleta unafuu hasa baada ya kutenga madirisha maalumu ya wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya tofauti na ilivyokuwa awali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika na Kiwwauta, Amina Mwinami anasema bado kuna kusuasua kwa kuundwa kwa mabaraza ya wazee katika ngazi mbalimbali hatua inayosababisha wazee kuendelea kukosa nguvu ya pamoja ya kujinasua kwenye changamoto zinazowakabili.

Chanzo: habarileo.co.tz