Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wa vigogo serikalini wachuana Chipukizi CCM

Siasaa Ccmmmmm.jpeg Watoto wa vigogo serikalini wachuana Chipukizi CCM

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar/Iringa. Watoto wa vigogo serikalini wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Chipukizi katika chaguzi zinazoendelea ndani ya jumuiya hiyo.

Kujitokeza kwa watoto hao kumeibua hisia gumzo mitandaoni ambapo baadhi ya watu wanahusisha kujitokeza kwao na wazazi wao huku wengine wakieleza kwamba ni haki yao kama watoto wengine wa Kitanzania.

Katika orodha iliyotolewa na UVCCM, walioteuliwa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Chipukizi Taifa ni Hytham Mwanyemba, Qailah Bilal, Neema Kinyonga na John Mpoto.

Chipukizi ni Idara ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) inayojikita katika kuwakuza na kuwalea watoto ili waje kuwa viongozi ndani ya chama hicho.

Walioteuliwa kugombea nafasi ya wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji ya Chipukizi ni Brianna Mahiga, Shamim Omary Haji, Ridhaa Mwambiko, Mussa Shabani Mussa, Hemed Makame Seleman, Simba Jerry Silaa, Zacheeus Ngeseyan, Rafat Ally Simba, Abdallah Faraj Abdallah na Anniyah Kiata.

Wengine walioteuliwa kugombea nafasi ya wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM – Bara ni pamoja na Isack Nchemba, Alvin Byabato, Bryan Mahiga, Koira Marigwa, Shamsa Aman Rashid, Mariekighei Joseph, Mussa Paul, Mussa Shabani Mussa na Rafat Simba na Alvin Rutainurwa.

Kwa upande wa Zanzibar, walioteuliwa kuwania ujumbe wa Baraza Kuu la UVCCM ni Ahfan aid Dimwa, Rukaya Maktuba Haji.

Akizungumzia kuhusu hilo, kada wa CCM, Joyce Juma amesema watoto wa viongozi ni watoto kama watoto wengine, hivyo wana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya UVCCM kama ilivyo sasa.

“Watoto wasinyimwe fursa au wasibaguliwe kisa wazazi wao ni viongozi. Hakuna mahali katiba imekataza mtu akiwa mtoto wa kiongozi asigombee. Pia, viongozi wakubwa kwa wadogo wote wana watoto.

“Tuwaache watoto wapate haki zao ila kuwa mtoto wa kiongozi haifanyi anyimwe fursa ya kugombea nafasi yoyote. Kikubwa ni kwamba haki ifuatwe,” amesema kada huyo.

Akiwa na mtazamo tofauti, Shukuru Mchokozi kutoka Iringa amesema anaona hatari mbeleni kwa wazazi kuingilia uchaguzi wa Chipukizi na kwamba anaona kizazi kijacho kikiharibiwa na wazazi wenyewe kwa kuwasukuma huko watoto.

“Nimekaa nikatafakari kwa kina sana, nikajiuliza hivi tunataka tujenge Taifa gani la kizazi cha baadaye kama tutaenda na mfumo huu wa Chipukizi kuingiliwa na wazazi, wanachama na viongozi wa UVCCM kwenye chaguzi zao.

“Naona tunajenga kizazi kibovu mbeleni kwa sababu ya sisi tulioharibika, ambao tumezoea ili tuingie kwenye uchaguzi lazima uwe na fungu la kuwakirimu wajumbe, bila kuwa na takrima hiyo huwezi kushinda,” amesema.

Naye Paschal Myovela amesema “wanaoomba kura kwa ajili ya vijana wa chipukizi wakumbuke pia kuwaombea watoto wa wakulima na wasio na wazazi wenye majina makubwa na wenye vipato vikubwa. Safari yao ya maisha yajayo na utabaka vinaweza kuumbwa sasa.”

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa Idara ya Hamasa na Chipukizi wa UVCCM, Edna Lameck amesema uchaguzi wa chipukizi umefika hatua ya kitaifa na viongozi wengine katika ngazi za mikoa wamekwishapatikana.

“Uchaguzi umefanyika nchi nzima na tayari viongozi wamepatikana ambao ndio wajumbe wa mkutano mkuu Taifa. Huu unakuwa mkutano mkuu wa nane wa Taifa, amesema Edna. Ameongeza kuwa Chipukizi ni moja kati ya idara zilizoko UVCCM inayohusika na watoto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live