Watendaji wa uchaguzi kwenye uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara uliotangazwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wametakiwa kuwashirikisha kwa ukaribu wadau wa uchaguzi kwenye maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele leo Februari 20, 2024 wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Uchaguzi huo utafanyika Machi 20, 2024 ambapo fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia Februari 27, 2024 hadi Machi 4, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 4, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Machi 5 hadi 19, 2024.
“Napenda niwakumbushe na kuwasisitiza kuwa, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi , ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema Jaji Mwambegele.
Pia, amekumbusha juu ya umuhimu wa kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa watendaji hao wa uchaguzi, kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura. Jaji Mwambegele alisisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya utambuzi na kukagua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Mwenyekiti huyo wa Tume amekumbusha juu ya wajibu wa kuhakikisha kwamba watendaji wa vituo watakao ajiriwa wanakuwa watu wenye weledi na wanaojitambua.
“Tuachane na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
“Mhakikishe siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo utahitajika ushauri kuhusiana na masuala ya uchaguzi,” Jaji Mwambegele aliwasisitiza watendaji hao.
Aliwakumbusha kuwa uchaguzi ni jambo la kisheria na kwamba sheria na taratibu zikifuatwa ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Hata kama umeshasimamia chaguzi kadhaa hapo nyuma, lakini uchaguzi huu mdogo unaojumuisha kata 23 haujawahi kuusimamia,” amesema.
Kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).
Nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).