Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wachukua fomu urais, Magufuli leo

C0ecac6253db4d1c5ae31b4ee40cd926 Watatu wachukua fomu urais, Magufuli leo

Thu, 6 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAGOMBEA wa vyama vitatu vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jana walifungua pazia la kuchukua fomu za kugombea kiti cha urais na Makamu wa Rais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Wagombea hao ni kutoka Chama cha Wakulima Tanzania (AAFP), Democratic Party (DP) na National Reconstruction Alliance (NRA). Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli leo anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi jijini Dodoma kuwania nafasi hiyo kwa mara ya pili.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ilieleza jana kuwa Magufuli atachukua fomu leo saa 3 asubuhi kwenye ofisi za makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Njedengwa akiwa amesindikizwa na watu wachache wakiwemo viongozi wakuu wa chama.

“Baada ya kuchukua fomu ndugu Magufuli atakwenda katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma (White House) ambako atakutana na wanachama, wapenzi na wakereketwa wa CCM na kuwasalimu” alieleza Polepole.

Awali jana, Polepole alisema jijini Dar es Salaam kuwa chama hicho kina imani kubwa kuwa mgombea huyo atashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo kutokana na utendaji wake kuwa wa mfano, si tu katika nchi za Afrika, bali duniani kwa ujumla.

Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mgombea huyo amefanya kazi kubwa katika awamu yake ya kwanza.

Mapema jana Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage aliwakabidhi fomu wagombea wa vyama vya AAFP, DP na NRA. Jaji Mstaafu Kaijage aliwapongeza wagombea hao kwa uthubutu wao na kuaminiwa na vyama vyao hadi kuteuliwa kugombea nafasi hiyo na aliwatakia kila la heri katika hatua zote lisema kuwa NEC imeandaa begi ambalo lina kitabu cha maelekezo ya vyama vya siasa na wagombea ikiwemo kitabu cha maadili, kanuni na sheria za uchaguzi.

Kaijage alisema kuwa wagombea wanakabidhiwa seti nne za fomu namba 8A ambazo ni fomu za uteuzi wa wagombea wa urais na makamu, ambapo kila seti kuna nakala 10 ili kuwezesha kupatikana idadi ya wadhamini wanaotakiwa. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Wilson Charles alisema kuwa wagombea hao watatakiwa kudhaminiwa na wapiga kura 2,000 kwa mikoa 10 na kwamba minane ni ya Tanzania Bara na miwili Zanzibar.

Kwenye kila mkoa wadhamini wanatakiwa wasipungue 200. Dk Charles alisema wagombea wa nafasi hizo watatakiwa kutoa tamko mbele ya Jaji na tayari NEC imeshawasiliana na Jaji Kiongozi kwa ajili hiyo.

Katika vyama vyenye usajili wa kudumu 19, vyama viwili TLP na UDP vilitangaza mapema kwamba havitasimamisha wagombea wa nafasi ya urais, vitamuunga mkono mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Rais Magufuli. Mgombea urais kwa tiketi ya AAFP, Seif Maalim Seif akiwa na mgombea mwenza wake, Rashid Rai waliahidi kuwa atafanya kampeni za kistaarabu.

Mgombea urais kwa tiketi ya DP, Philip Fumbo akiwa na mgombea mwenza wake, Zaina Juma Khamis alisema kuwa utaratibu wa uteuzi bado, hivyo kwa sasa wametekeleza suala la kisheria la kuchukua fomu na wanakwenda kutafuta wadhamini.

Chanzo: habarileo.co.tz