Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watasema nini baada ya Lowassa kurudi CCM?

46161 LOWASAAA+P Watasema nini baada ya Lowassa kurudi CCM?

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miongoni mwa viongozi wa vyama ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakichafuliwa na kusafishwa na watu haohao ni pamoja na Edward Lowassa.

Wakati akiwa CCM kabla ya kutimkia Chadema Julai 28, 2015 alikuwa akinangwa kwa ufisadi, papo hapo alipohamia Chadema aliendelea kuitwa fisadi na watu wa CCM huku watu wa Chadema wakimsafisha, lakini hivi sasa amerudi CCM watasema nini?



Mnamo Septemba 29, 2015 Humphrey Polepole akiwa kwenye kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Channel 10 alisema Lowassa ni tajiri hana uhusiano na masikini na hahitaji kusafishwa kisheria kama ambavyo Chadema walikuwa wanadai kwamba kama ana hatia ya ufisadi inayosemwa apelekwe mahakamani.

Alitoa kauli hiyo mara baada ya kiongozi huyo kuhamia Chadema na chama hicho kutumia nguvu nyingi kumsafisha kutoka kwenye dimbwi la tuhuma za ufisadi alizokuwa akishutumiwa.

Kwa upande wa katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba alikuwa akieleza udhaifu wa Lowassa katika mikutano ya kisiasa wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015.

Related Content



Akiwa kwenye kampeni sehemu mbalimbali aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Makongoro Nyerere alisema Tanzania inakabiliwa na tatizo la ufisadi na rushwa.

Alisema kwa kuwa ufisadi bado ni tatizo, wataendelea kuwaeleza Watanzania katika kampeni zao kuwa mgombea huyo wa Chadema ni fisadi.

Lowassa amekuwa na nia ya kugombea urais kwa muda mrefu tangu mwaka 1995 wakati jina lake lilipokatwa, hakuchukua fomu mwaka 2005 wakati Jakaya Kikwete, aliyekuwa rafiki yake wa karibu, alipogombea.

Lowassa alisema walikubaliana na Kikwete kwamba waunganishe nguvu ili awamu inayofuata iwe zamu ya mbunge huyo wa Monduli.

Hata hivyo, mwaka 2015 jina la Lowassa lilikatwa na makada wengine 33 na ndipo akaamua kujiunga na Chadema kuendeleza ndoto yake ya kuingia Ikulu.

Septemba 29, 2015 aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCM, Nape Nnauye akiwa kwenye  viwanja vya Samora, mjini Iringa alitumia dakika 10 kumshambulia Lowassa.

Alisema Lowassa ni mwizi na fisadi na kwamba hakuna sehemu ambayo alipewa kufanya kazi katika ngazi za CCM na Serikali bila kuiba.

 

Nape alidai Lowassa alishindwa kukaa CCM kwa kuwa hawezi kufugika "Lowassa ni  kunguru, hafugiki."



Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita ambaye sasa ni mbunge wa Geita, Joseph Msukuma naye alimvaa Lowassa alipohamia Ukawa kwa kusema kuwa wanashukuru chama kimetua mzigo.

“Nataka nimwambie ndugu yangu, rafiki yangu Lowassa, huu ni muziki mkubwa,” alisema Msukuma kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa urais wa CCM, Dk John Magufuli uliofanyika mjini Chato, mkoani Geita Septemba 21, 2015.

“Tunaomba wachukue na wengine wenye tabia kama hizo. Wenye akili timamu tutabaki CCM...Mgombea wetu (Magufuli) anatosha. Na hapa ndiyo kwao, nimetembea na Lowassa gari moja, ndege moja, tunachagua rais na sio bora rais,” alisema.

“Katika Kanda ya Ziwa, hakuna aliye na siri za Lowassa kama mimi, naomba waniweke kwenye mdahalo nitagharimia, niwapige kavu kavu. Watu wanaokwenda kule (Ukawa) zinatangulizwa hela. Nani anachukia hela?.”

Mara baada ya Lowassa kwenda Ikulu kuzungumza na Rais Magufuli, Msukuma alibadilika na kumuasa kuwa, “Mi nakuomba Mzee Lowassa huku ndiyo kwenu hilo genge la wahuni hutoliweza, Lowassa kwenda kule ilikuwa ni hasira tu.”



Naye Dk Harrison Mwakyembe akiwa Waziri wa Afrika Mashariki, alitoa andiko la kujiapiza kupambana kufa na kupona kuhakikisha Lowassa haingii Ikulu.

Katika andishi lake alilolituma kwenye mitandao ya kijamii, Dk Mwakyembe anasema, Lowassa hana sifa ya kuwa Rais.

“Namuona Lowassa kama mtu ambaye anatapatapa huku akiujua ukweli kwamba hana nafasi hata kiduchu ndani ya CCM.”

Alisema anahaha kutumia mabilioni kuhonga na kusafirisha watu kwenye tendo la kutangaza nia tu, hivi unafikiri kamati zote za CCM zina njaa ya pesa zako za kifisadi?

Dk Mwakyembe ambaye sasa ni waziri wa habari, utamaduni, Sanaa na Michezo alisema atakuwa wa kwanza kujitafakari na kuitafakari CCM na kuchukua hatua ambayo najua Watanzania wasiouza utu wao kwa dhamana ya fedha.

“Ninakusubiri kwa hamu ili nikusikie utakavyokuwa unabadili jahanam kuwa peponi, kwa manufaa ya Watanzania nitaanika hadharani uozo wako wote kwa ujasiri na bila hata chembe ya woga ili Watanzania wasipotoshwe tena kwa njia ya bwembwe za fedha,” alisema.



Kiongozi wa ACT- Wazalendo Zitto Kabwe akiwa Singida kwenye mkutano wa kampeni Agosti 7, 2015 alisema ni kazi ngumu kumsafisha Lowassa kutokana na kuwa na kashfa za ufisadi.

Hizi ni baadhi ya kauli za wanasiasa hawa kuhusu Lowassa, swali linabaki kwa sasa baada ya kurejea CCM watakuwa na kipi cha kusema juu ya mwanasiasa huyu?



Chanzo: mwananchi.co.tz