Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasomi wataja siri anguko la wateule ubunge CCM

1ff7040a946732da3b5857b94fe5205b.jpeg Wasomi wataja siri anguko la wateule ubunge CCM

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WACHAMBUZI wa siasa na wasomi wamesema kushindwa kufanya vizuri kwa baadhi ya waliokuwa wateule wa Rais John Magufuli kwenye kura za maoni, kwa walioomba kupitishwa kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumechangiwa na mambo mengi, ikiwemo uwezo wa wanaCCM kuwapima wagombea bora wanaowataka.

Mtaalamu wa mambo ya siasa katika Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala, alilieleza HabariLeojana kuwa wanaCCM wanafahamu ni mgombea yupi anawafaa.

Kwa mujibu wa Profesa Mpangala, baadhi ya waliokuwa wateule wa Rais Magufuli wameshindwa kuongoza kwenye kura za maoni, kwa kuwa wanachama wa CCM wanafahamu wagombea wanaowataka.

“Kwa kuwa walikuwa wateule wa Rais katika nafasi za uongozi walizokuwa nazo, nafasi hizi ni kubwa na walikuwa wanahusiana moja kwa moja na wananchi, kwa hiyo kupitia nafasi hizo, wananchi nao walikuwa na nafasi ya kuwapima,”alisema.

Mtaalamu wa mambo ya siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Richard Mbunda, alisema kutokufanya vizuri kwenye kura za maoni za CCM kwa wateule hao wa Rais, kunategemea na namna walivyowekeza imani katika majimbo waliyogombea.

Profesa Mbunda alisema mbali na kutowekeza imani ya kutosha ya kufanya vizuri kwenye kura za maoni, inawezekana pia wateule hao hawakufanya tathmini ya kutosha, kujiridhisha kiasi gani wanakubalika kwenye majimbo walikoenda kuomba wagombee ubunge.

Alisema pia inawezekana kutofanya vizuri kwao, kumechangiwa na mchakato wa kura za maoni ulivyokuwa mwaka huu. Profesa Mbunda alisema mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM mwaka huu ulihusisha wajumbe wachache, tofauti na miaka ya nyuma.

Jambo lingine ambalo Profesa Mbunda alilitaja kuwa huenda limechangia kushindwa kufanya vizuri kwa baadhi ya wateule wa Rais, ni upeo mkubwa wa kufikiri wa watu katika majimbo ya mjini.

Alisema kuwa wateule hao walitahadharishwa mapema kutogombea wakiwa bado katika nafasi zao za uongozi, lakini hawakusikia. Hivyo, matokeo hayo yanaweza kuwa sababu ya wajumbe kuwaadhibu kupitia sanduku la kura, baada ya kuona ni watu wasiotosheka.

Kwa mujibu wa Profesa Mbunda, viongozi wakuu wa kitaifa wa chama, ni kama vile waliwasemea kwa wananchi, kwamba wateule hao walipewa majukumu lakini hawakutosheka, hivyo kutaka majukumu mengine.

Mtaalam mwingine wa mambo ya siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohamed Bakari alisema uamuzi wa wateule hao kugombea nafasi za ubunge, haukuwa wa kukurupuka, bali walijiandaa.

Profesa Bakari alisema utaratibu mpya wa CCM wa kuhesabu kura za maoni hadharani ni mzuri, kwa kuwa unajenga imani kwa wanachama na kupunguza migogoro. Baadhi ya waliokuwa wateule wa Rais ambao hawakuongoza katika kura za maoni katika majimbo waliyogombea ni Kipi Warioba, Paul Makonda, David Kafulila, Patrobas Katambi.

Kipi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Makonda alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kafulila alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe na Katambi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma. Tayari Rais ameteua viongozi wengine kuchukua nafasi za watu hao.

Chanzo: habarileo.co.tz