KUENGULIWA kwa wagombea ubunge sita kati ya 11 mkoani Morogoro kumechangiwa na kushindwa kwao kutimiza takwa la kisheria katika fomu za kuomba uteuzi wa ubunge zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Majimbo sita wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walipitishwa kuwa wagombea pekee wa ubunge baada ya wagombea kutoka vyama vya upinzani kutokidhi matakwa ya kisheria katika fomu za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea halali.
Kwa upande wa Msimamizi wa Jimbo la Gairo, Agnes Mkandya akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, alitaja mambo ya kisheria walioshindwa wagombea wa jimbo hilo ukiacha CCM kuwa ni fomu zao kutosainiwa na kugongwa muhuri pamoja na wengine kushindwa kurejesha fomu kwa muda muafaka ambao ni saa 10 jioni.
“Pamoja na kwamba walitangulia kuchukua fomu za kuomba uteuzi kwa wabunge kuanzia Agosti 12 na wengine 13 na 14 , mwaka huu bado walioshindwa kutimiza matakwa yaliyowekwa na Tume ili wateuliwe tofauti na mgombea wa CCM aliyechukua fomu kati ya Agosti 21, na kurudisha zikiwa hazina kasoro. Wanakosea wao wenyewe ili waelekeze lawama kwa wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo," alisema Mkandya.
Naye, Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Morogoro mjini, Sheilla Lukuba akitangaza juzi kuhusu urejeshaji wa fomu za wagombea wa ubunge za wagombe watano wa Jimbo hilo, alisema kuwa ni mgombea mmoja pekee wa CCM , Abdulaziz Abood alikidhi matakwa ya Sheria kwenye fomu zake.
Wagombea wenzake wanne walishindwa kuteuliwa kuwa wagombea katika jimbo hilo baada ya kushindwa kukidhi matakwa hayo.
Hata hivyo, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Kilosa na anayesimamia majimbo mawili ya Morogoro kusini pamoja na Morogoro kusini mashariki hawakuweza kupatika kuzungumzia kiini cha wagombea wa vyama vya upinzani kutokidhi matakwa ya kisheria ya NEC.
Wagombea wa CCM waliokosa upinzani katika majimbo yao ni Abood (Morogoro mjini),Hamis Taletale (Morogoro kusini mashariki), Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa), Ahmed Shabiby (Gairo),Jonas Vanzeeland (Mvomero) na Innocent Kalogeris (Morogoro kusini).