Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasaliti kufukuzwa CCM

695d55f8177a71205425f7e85f8b5a7f Wasaliti kufukuzwa CCM

Wed, 3 Aug 2022 Chanzo: Habari Leo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetaka wanachama wake wawafukuze wasaliti ndani ya chama na wasiwapokee baadaye wanapodai wamejirekebisha.

CCM imesema hakuna uhakika kwamba msaliti huyo amejirekebisha hivyo hakuna sababu ya kumpokea kwani uwepo wake ndani ya chama ni hasara kwa kusababisha kushindwa uchaguzi.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo alisema hayo Jumatatu wakati anazungumza na wanachama wa chama hicho eneo la Bomang'ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

"Mwaka 2015 nilipita wilaya hii wakati wa Uchaguzi Mkuu wa madiwani, ubunge na Rais, jinsi watu walivyokuwa wanajaa katika mikutano huwezi tegemea matokeo yake," alisema Chongolo.

Alisema uimara ndani ya CCM hautokani na kuvaa mavazi ya kijani ila kuwa na wanachama wenye mapenzi mema na kukisaidia chama katika uchaguzi.

Chongolo alisema hakuna mwanachama au kiongozi mkubwa kuliko chama na kwamba kinachohitajika ni kukisaidia nyakati zote.

"Jeshini wao wana utaratibu wao, mtu akiwa msaliti adhabu yake ni kifo, maana uwepo wake ni hasara kuliko kukosekana kwake...sisi huku tunakufukuza na hatukupokei tena," alisema.

Chongolo alisema jambo la kushangaza ni pale ambapo mwanachama mmoja akikosa nafasi anayoomba ndani ya CCM anageuka kuwa adui na kutaka chama chote kishindwe uchaguzi.

Katika matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Tanzania, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Marehemu Dk John Magufuli alipata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46.

Alisema aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97.

Kuhusu chakula, Chongolo alitahadharisha wananchi wa Hai wahifadhi chakula na wasikitumie kutengenezea pombe za kienyeji kwa sababu msimu huu wa mavuno umekuwa na changamoto ya ukame ulioathiri mavuno.

"Nchi nzima tuna changamoto ya mvua, kumekuwa na ukame, wito wangu kwenu kila mmoja ahifadhi chakula alichopata msimu huu tutumie vizuri akiba hiyo, hifadhi chakula msipikie pombe au msiuze," alisema Chongolo.

Chanzo: Habari Leo