Waziri Mkuu mstaafu, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesimulia alivyomshauri hayati Edward Lowassa alipokutana na misukosuko ya kisiasa na kuamua kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008.
Warioba amesema baada ya kusikia jambo hilo, alizungumza na Lowassa na kuhoji kama hakupewa nafasi ya kusikilizwa, hata hivyo amesema alimshauri kwa kitendo cha kutuhumiwa, ilikuwa ni muhimu kujiuzulu.
Jaji Warioba amesema hayo leo Jumanne, Februari 13, 2024 wakati akitoa salamu za pole kwa Taifa na familia ya Lowassa, wakati wa kuaga mwili wa kiongozi huyo mstaafu katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
"Alipojiuzulu alinifuata akasema, hakutendewa haki, wamemuhukumu bila kumsikiliza, nilitoa tamko nikasema kama kweli ni hivyo basi hawakumtendea haki," amesema.
Warioba amesema hata hivyo alimwambia kuwa hayo ni mambo ya kisiasa, hata kama wangemsikiliza bado ilibidi aachie ngazi kutokana na kuhusishwa na tuhuma hizo.
Warioba ameongeza pia kuhusu kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, alimshauri apunguze spidi lakini alisimamia vipaumbele vyake.
"Nakumbuka kipindi ambacho tunataka sana watoto wote waende shule, kipindi hicho hatuna madarasa, walimu, vifaa vya elimu vya kutosha, nilikwenda kumshauri apunguze spidi, alisema hapana, hapa ndipo pa kuanzia (ujenzi wa shule za sekondari za kata).
"Alikuwa na maono yake, vipaumbele vyake, hakuwa mangi meza, alifanya kazi saiti pamoja na kwamba alikuwa binadamu naye ana mapungufu kama wengine, lakini hakutaka kugombana na watu,”amesema Warioba.
Licha ya Warioba kukiri kutokuwa na ukaribu sana na Lowassa, lakini mara kadhaa aliombwa ushauri na kiongozi huyo aliyefariki Februari 10, 2024. Warioba asimulia alivyomshauri Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu
Vilevile, Jaji Warioba amesema miongoni mwa mambo ambayo anamkumbuka Lowassa ni pamoja na mwaka 1995 ambapo yeye (Lowassa) pamoja na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete walipoingia kwenye kinyang'anyiro cha kuomba ridhaa ya chama kugombea urais.
"Hakuvuka kwenye kamati kuu aliumia, lakini aliumia zaidi alipojua aliyepigilia msumari ni Mwalimu Nyerere, alikuja kwangu akasema hakusikilizwa na ameaumia zaidi mwalimu kutia msumari, nilimwambia hayo yasikuvunje moyo wewe bado ni kijana na una muda.
"Nilimwambia aende amuone Mwalimu, akasema nitamfikiaje, pale pale nikampigia msaidizi wake, alikwenda wakazungumza,”amesema.
Alama zitakazokumbukwa
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema hayati Lowassa ameacha alama Tanzania ambazo zitakumbukwa daima.
“Jana nilipata nafasi ya kuzungumza mengi kuhusu mpendwa wetu nyumbani kwake nilipoenda kuhani na viongozi wenzangu walionitangulia, nirudie kutoa pole kwa Mama Regina Lowassa (mjane) na familia yote ni msiba wa Taifa letu lote kama ilivyojidhihirisha,” amesema Kikwete.
Kikwete ameomba wote wawe na moyo wa subira na ustahimilivu, kwani kifo kimeumbwa na Mungu kama alivyoumba uhai.
“Sisi wote ni waja wake na kwake tutarejea. Tunamshkuru Mungu kwa muda aliotupatia kuishi, muda wa uhai wake alifanya maendeleo mengi kwa nchi yetu na ameacha alama zitakazokumbukwa daima.
“Shukrani kubwa tunayoweza kutoa kwake kwa sasa ni kumuombea kwa mola aiweke roho yake mahala pema peponi, Mungu ametoa na ametwaa,” amesema Kikwete.
Mwili wa Lowassa unatarajiwa kuzikwa Februari 17, mwaka huu kijijini kwao Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.
- Kisa cha Diana Chilolo kufuta namba ya Lowassa
- Tazama hapa msafara wa mwili wa Lowassa ukipelekwa Karimjee
- Shein, Sumaye waeleza uchapakazi wa Lowassa
- Picha: Matukio mbalimbali katika zoezi la kuaga mwili wa Lowassa
- Fredy Lowassa: Asingekuwa Rais Samia, baba asingefika juzi
- Read all related articles