Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Warioba aanika kasoro hizi uchaguzi 2020

Wariobaa12 Jaji Joseph Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema kasoro ziliojitokeza kwenye Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 lazima zijadiliwe kwa uwazi ili kuepeuka kujirudia kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2025

Pia ameeleza kushangazwa na watu wanaoogopa kujadili kasoro hizo waziwazi, akionya kuwa kitendo hicho kinafanya uchaguzi kuwa wa viongozi na vyama na siyo wananchi ambao ndiyo wanapiga kura.

Jaji Warioba aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Vyombo vya Habari na Uchaguzi 2020, Ubora wa Maudhui ya Vyombo hivyo Tanzania, uliofanywa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema imefika mahali watu wanaogopa kuzungumzia hitilafu zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, huku akivinyooshea kidole vyombo vya habari kwa kutokufanya uchambuzi kuonyesha kasoro hizo.

Alitoa mfano kuwa aliwahi kufanya kazi idara ya sheria serikalini na ilikuwa ni kawaida kila baada ya uchaguzi kubaini kasoro na kufanya tathmini ili zisijirudie na ndiyo maana sheria na kanuni za uchaguzi zimekuwa zikifanyiwa marekebisho.

“Tumefika mahali tunaogopa kuzungumzia hitilafu tulizoziona kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, ni kawaida uchaguzi wowote utakuwa na hitilafu kokote duniani, imefika mahali tunaogopa kuzungumzia hitilafu tulizoziona kwenye mchakato wa uchaguzi.

“Uchaguzi uliopita ulikuwa na hitilafu nyingi sana na zilionekana wazi. Kwa mara ya kwanza nchi hii ilikuwa kama ndiyo tunaanza uchaguzi, hatukuzoea.”

"Kwa mara ya kwanza watu (wagombea) wengi wameenguliwa tangu mwaka 1961 nchi ipate uhuru, kasoro zilijitokea nyingi sana lazima tutafute sababu ili yasijirudie.

“Kwa sasa tuzungumze haya (kasoro) yasitokee tena lakini watu wanazungumza chini chini wanaogopa kuyasema, hapana! Lazima tuzungumze tujue uchaguzi ni wa wananchi na taratibu tutakazokuwa nazo ziwe za wananchi na siyo viongozi,” alisema.

VYOMBO VYA HABARI

Jaji Warioba alisema vyombo vya habari vinatoa habari nyingi lakini bado inahitajika kazi kubwa kwa waandishi kutoa taarifa za kusaidia wananchi badala ya kuwa wanaripoti matukio ya watu.

“Katika ripoti hii tumeona wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 watu walisikiliza na kuangalia na kusoma habari za kampeni kila siku, ni kipindi ambacho wananchi wengi wakati wa taarifa ya habari wanataka wasikilize, lakini ukiona taarifa zinazopewa kipaumbele.

“Vyombo vya habari havikutoa taarifa muhimu za kusaidia wananchi, huwa najitahidi kujua msimamo wa viongozi na vyama mbalimbali wakati wa uchaguzi.

"Tuliingia uchaguzi wa 2020 ilani za vyama vya siasa hazikuwa zinapatikana kwa urahisi, wananchi walitegemea kutoka kwa wagombea lakini kufahamu sera za vyama ilikuwa ngumu maana hazipatikana ila vyombo vya habari vilikuwa na ilani vilipaswa kufanya uchambuzi ili wananchi waelewe,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, vyombo vya habari vinajielekeza zaidi kuwaandika viongozi na kuwaacha wananchi, jambo ambalo limejitokeza kwenye ripoti hiyo.

“Tunaona viongozi na serikali ndiyo habari tunasahau wananchi, nilitegemea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 maoni ya wananchi yangeonekana kuanzia hatua za uteuzi lakini hayakuonekana licha ya kwamba uchaguzi ni wa kwao,” alisema.

Jaji Warioba alisema sababu zinazoelezwa ni weledi ambalo ni jukumu maalumu la kuwafunza waandishi wawe na ujuzi zaidi, na sababu nyingine ni uchumi ambayo ni lazima wawe na ubunifu kujitengenezea mapato kwa kupunguza kutegemea matangazo kutoka serikalini.

Alisema aliwahi kufanya kazi kama mwandishi wa habari kwenye gazeti la Standard ambalo kwa sasa ni Daily News na hawakuwa na mafunzo ya uandishi wa habari, lakini walifundishwa namna ya kuandaa habari na kufanya utafiti.

“Nimesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kilikuwa kinasifika kwa kutoa mawazo makubwa, sasa wanahabari wanasema kuna woga unatokana na nini?".

"Mhariri mmoja aliwahi kunieleza kwa kina kwamba 'Mzee tukiandika mambo ya kuudhi mahali fulani tunafungiwa, unakuta mlalamikaji ni huyo, mwandaaji mashkata ni huyo, anayehukumu ni huyo huyo.

“Niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), tulisikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu vyombo vya habari na tulikuwa tunafanya wazi kila mtu anaridhika, malalamiko yalikuwa yanaletwa waziwazi,” alisema.

“Kuna taasisi nyingi (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Msajili wa Magazeti zimepewa madaraka, zinayatumia bila uwazi na wakati mwingine zinatoa adhabu kubwa kabisa kuliko ambazo zinatolewa na mahakama.

"Nchi haiwezi kuendelea kama watu wake hawana uhuru... Tunaweza kuwa na maendeleo ya vitu lakini kama watu hawana uhuru wa kutoa mawazo yao hayo siyo maendeleo,”alisema.

Akiwasilisha utafiti huo, Mtafiti kutoka SJMC, Dk. Abdallah Katunzi, alisema vyombo vya habari binafsi viliripoti habari za uchaguzi mkuu kwa wagombea urais kwa asilimia 64 mgombea urais wa CCM na asilimia 42 mgombea wa CHADEMA.

Alisema kwa Zanzibar vyombo vya Tanzania Bara viliripoti kwa ulinganifu kuliko vilivyopo visiwani humo.

Alisema kwa ujumla vyombo vya habari havikuripoti sera za vyama badala yake viliripoti yaliyokuwa yakisemwa na wagombea huku CCM ikiripotiwa zaidi kuliko upinzani.

“Mazingira kabla na baada ya uchaguzi hayakuwa rafiki kwa vyombo vya habari, Gazeti la Tanzania Daima lilifutiwa usajili kabla ya kuanza uchaguzi huku Clouds Radio na TV wakifungiwa kwa siku saba lakini serikali ilitoa sababu,” alisema Dk. Katunzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live