Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Warioba: Utoaji maoni Katiba mpya usiwaache wananchi

7e8db3be0ce8edc7a9e3ad3ed4136b3e.jpeg Utoaji maoni Katiba mpya usiwaache wananchi

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema mabadiliko ya Katiba ni utashi wa kisiasa, lakini kwa kuwa mchakato wake umetoka mbali ni lazima utafikia mwisho. Alisema hayo jana Dar es Salaam baada ya kutoa maoni mbele ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupokea maoni kuhusu demokrasia, mikutano ya vyama vya siasa, rushwa na mengineyo.

Alisema hivi sasa maoni yanayotolewa kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya mengi yameegemea upande wa viongozi na kuwaacha wananchi suala alilosema si sahihi kwa kuwa Katiba ni ya watu wote. “Ifike mahali viongozi wetu waweze kukubaliana ili tuwe na Katiba mpya ambayo itazingatia maoni ya wananchi, hili ni suala muhimu ambalo tumesisitiza wakati wote,” alisema Jaji Warioba.

Alisema anachokiona sasa ni maoni mengi yanawahusu viongozi na wasomi na kuwaacha wananchi jambo ambalo si sahihi. Kuhusu suala la amani, Jaji Warioba alisema anaona viashiria vya ukabila, udini na ukanda na hivyo kupoteza dhana iliyokuwa imewekwa na waasisi wa taifa kujenga umoja wa kitaifa.

“Waasisi walijenga taifa hili tukawa na umoja, tukawa na amani kwa kuondoa udini, ukabila na ukanda vitu ambavyo kwa sasa naona vinarudi kwa nguvu, imefanya watu wengine washindwe kuaminiana, tusijetukarudi tulikotoka,” alisema.

Awali, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula alisisitiza suala la maridhiano ili kuondoa kadhia zinazojitokeza baina ya vyama vya siasa na kueleza kuwa hakuna linaloshindikana mbele ya meza.

Alisema amekuwa mshirika katika suala hilo kwa kipindi kirefu akishiriki vikao mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuwapo kwa maridhiano kwa maslahi mapana ya taifa. Kuhusu Katiba, alisema suala hilo siyo jipya kwani lilianza muda mrefu tangu mwaka 1961, hivyo hakuna tatizo lolote juu ya mchakato wake hasa kama utazingatia maelewano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live