Moshi. Mgombea udiwani kata ya Mawenzi kwa tiketi ya chama cha Sauti ya Umma (Sau), Issack Kireti jana Agosti 9, 2018 alikuwa kivutio cha aina yake baada ya wapita njia kuamua kumfanyia kampeni.
Wapita njia wasiopungua watano waliokuwa wakipita eneo la Posta alilokuwa akifanyia mkutano, waliamua kuchukua kipaza sauti alichokuwa akikitumia na kuanza kumnadi kwa wananchi.
Hali hiyo na ahadi za mgombea huyo ikiwamo ahadi mpya ya kuwalisha wananchi wake kuku kila Jumamosi ya kila mwezi ili wapate afya njema, ilionekana kuwavunja mbavu waliokuwa wakimsikiliza.
Mgombea huyo, aliingia katika eneo la mkutano kwa kutumia pikipiki ya kukodi maarufu kama bodaboda, na mara baada ya kushuka alianza kuhutubia akiwakaribisha wananchi wamsikilize.
Vijana waliokuwepo eneo hilo na waliokuwa wakipita, walianza kumshangilia kwa maneno “Diwani, Diwani,Diwani,”na baadhi yao kuchukua kipaza sauti na kuanza kumnadi wakitaka achaguliwe.
Akihutubia katika mkutano huo, mgombea huyo amesema endapo atachaguliwa kuwa diwani, atahakikisha kila Jumamosi ya kila mwezi, kila kaya inapata kuku mmoja ili kuimarisha afya zao.
Mbali na ahadi hiyo, amerejea ahadi yake ya kujenga gereza la ghorofa kwa ajili ya wafungwa wa ufisadi na rushwa, akisema ataliweka swimming pool (bwawa la kuogelea), televisheni na wataruhusiwa kukutana na wenza wao.
Pia ameahidi kuendeleza kampeni yake ya kupanda miti aliyoianza tangu 2015, na pia atapambana na wizi wa Kanyaboya na kuwatafutia wafanyabiashara ndogondogo eneo la kufanyia biashara.