Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapinzani wavua kofia kwa Samia

1d9989d6234cebc2f40234f839e88bf4.jpeg Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wadau wa demokrasia nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kauli zenye lengo la kuwaunganisha Watanzania na wamehimiza kila mtu aheshimu Katiba ya nchi, sheria na kanuni.

Jumatano, Rais Samia alitoa mwito kwa wadau hao wazike tofauti zao, wafungue ukurasa mpya na kama kuna changamoto wazijadili kwa manufaa ya nchi. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya alisema CUF walikuwa wakiitafuta fursa ya kujadiliana, kushauriana, kuelekezana na kufikia hatma ya kuendelea kudumisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

“Fursa hii imetolewa ili yeyote aliyeona kama kuna shida mahali au changamoto au pale ambapo tuliona tulikuwa tunahitilafiana na serikali, vyombo vya dola, taasisi mbalimbali, tujadiliane ili tutoke na msimamo na kuja na utaratibu mzuri wa namna gani ya kuendesha demokrasia ya vyama vingi ndani ya nchi yetu kwa amani, utulivu, mshikamano na umoja,” alisema Sakaya.

Mkutano wa Dodoma unahudhuriwa na wadau wa demokrasia kutoka makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wastaafu nchini, wahadhiri wa vyuo vikuu, wachambuzi, taasisi za dini, taasisi za haki za kiraia, viongozi wa kisiasa na Baraza la Vyama vya Siasa.

Sakaya alisema miongoni mwa changamoto zinazofanyiwa kazi kwenye mkutano huo ni kukumbushana na kuelezana kuwa vyama vyote vya siasa viko kikatiba na kisheria, na kila chama kina wajibu wa kufuata katiba, sheria na kanuni.

Pia alisema msingi wa kuwepo vyama vingi si ugomvi, bali ni mfumo uliokubaliwa na Watanzania wenyewe japo walikuwa wachache, lakini wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere waliona umuhimu wa kuwepo kwa vyama vingi kwa kuwa ndiyo mfumo ulioingia duniani na hakukuwa na namna ya kuukwepa.

“Vyama hivi vina watu, haviongozi wanyama, punda, ngedere, vinaongoza watu, na hao watu ni Watanzania ambao wanataka haki zao za msingi ziheshimiwe na zipatikane, kwa hiyo vyama ni kama njia tu, lakini wanaodai hizi haki ni Watanzania,” alisema Sakaya.

Aliyekuwa Mgombea Urais kupitia chama cha ADC ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga alisema uamuzi wa Rais Samia wa kutaka changamoto zijadiliwe ni jambo jema kwani ni fursa kubwa kwa wanademokrasia wa kweli. Sendiga alisema anaamini taifa linakoelekea kwa sasa kutakuwa na siasa bora, ushirikiano na upendo. “Kauli za Rais za jana (juzi) ni za ukomavu mkubwa wa kisiasa, uungwana, kiuongozi, za umama kwa sababu amewakumbusha watu majukumu yao ambayo kimsingi ni ya kwao,” alisema Sendiga.

Aliongeza: “Ukiangalia watu wanaolalamika sana ni wale wanaotaka kutumia uhuru wao na uhuru wa wengine kitu ambachohakipo, kila mtu afuate sheria, yaani cheza kwa stepu usimkanyage mwenzio, cheza kwenye kieneo chako, hakuna nchi inayoendeshwa kama gheto la masela, lazima sheria zifuatwe.”

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Godwin Amani alisema watu wengi wanachanganya wakidhani demokrasia maana yake ni uchaguzi tu, bali ni mchakato unaojumuisha vitu vingi ikiwemo haki, uhuru, umoja, vyama vya siasa kufanya siasa bila kuingiliwa na uchaguzi wenyewe.

Aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia Makini, Cecilia Mmanga alisema wito wa Rais ni sahihi kwa sababu tofauti zinakuwepo kipindi cha uchaguzi, lakini baada ya hapo watu wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu kila mtu anagombea siyo kwa maslahi yake binafsi bali kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live