Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapinzani watapata tabu sana-Pinda

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Mizengo Pinda amewataka wananchi wa jimbo la Ukonga kumchagua Mwita Waitara ili aunganishe nguvu za kuleta maendeleo zilizojazana ndani ya Serikali ya CCM.

Pinda ambaye ni waziri mkuu mstaafu wa awamu ya nne, alisema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika jimbo la Ukonga zilizofanyika jana eneo la Kivule Shule.

Alisema Waitara alipokuwa upinzani haikuwa rahisi kwake kuonana viongozi wa Serikali, lakini kwa kuwa yuko CCM amepata marafiki wengi watakaomsaidia kutatua kero za wananchi wa Ukonga.

Pinda ambaye aliteuliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli kuwa mjumbe wa NEC aliwaeleza wananchi wa Ukonga kuwa mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Kitunda suala lake limeanza kufanyiwa kazi na yeye (Pinda) atakuwa ‘mpambe’ wa kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Aliwaeleza wananchi kuwa Waitara ni muhimu kwao kwa kuwa sasa anaungwa mkono na viongozi wa wilaya, mkoa na taifa, hivyo matatizo ya wananchi yatashughulikiwa kwa haraka.

“Upo bungeni unasimama kumnanga waziri mkuu kisha unamfuata pembeni unamuomba mradi wa maji atakuambia analifanyia kazi, kumbe kakuacha na yeye ni binadamu anataka heshima,” alisema Pinda.

Aliwataka wananchi wawaeleze wapinzani kuwa tabia yao ya matusi na kelele za unafiki itawafanya wasubiri sana na watapata tabu sana.

Pinda alitaka mabalozi wa nyumba 10 waheshimiwe kwa sababu wao ndiyo wameshika mizizi ya chama.

“Mabalozi tembeeni nyumba kwa nyumba kuhakikisha mnamtafutia kura Waitara,” alisisitiza Pinda.

Mjumbe mwingine wa NEC, Makongoro Nyerere akimnadi mgombea wa CCM, alisema yeye na Pinda walikuwa ‘benchi’ lakini Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli akawateua kuwa wajumbe wa NEC.

Alisema yeye pia alikuwa upinzani ambako alisota kwa miaka saba bila kuteuliwa hata ukatibu kata. Makongoro alikuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi.

Lakini aliamua kurudi CCM na aliweza kupata nafasi za uongozi ikiwamo mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara. Alisema mambo yaliyokuwa yakimkera alipokuwa upinzani ni hoja zisizo kwisha za ufisadi, rushwa na upendeleo.

Makongoro ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere ambaye ni Baba wa Taifa, alisema mafisadi na wala rushwa walikuwapo CCM lakini walishughulikia na vyombo husika.

Alisema wapinzani wakati wote walikuwa wanalalamikia mambo ya ufisadi wakimtaja sana Edward Lowassa, lakini alipowafuata wamekaa kimya na wanamsifia.

Mgombea ubunge wa CCM, Mwita Waitara alisema wakati Magufuli akiomba kura za urais alikuwa akionyesha ilani iliyosheheni, lakini Lowassa aliomba kura kwa kuonyesha makaratasi ambayo hayakuwa na kitu.

Alisema alikuwa akipata shida kuhusu matumizi ya ruzuku ya chama kwa kuwa wao kama viongozi walilazimika kujilipia kila kitu kwenye shughuli za chama.

“Kukiwa na mkutano malazi, chakula, usafiri, walinzi na kuchapisha nyaraka yoyote utajilipia mwenyewe na kampeni ya uchaguzi utafanya kwa gharama zako, haya yalinishinda,” alisema.

Alisema akiwa kama mbunge jukumu lake ni kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya, elimu, maji, shule na barabara,

“Ili nipate hayo lazima niongee na watu wa CCM kwa sababu ndiyo wanakusanya kodi na ndiyo wenye ilani ya kuendesha Serikali,” alisema.

Waitara alisema viongozi wake wa Chadema walimtaka kila anaposimama bungeni anatakiwa kuitukana Serikali, jambo ambalo lilimshinda.

Alidai kuna wakati walikuwa wanapangiwa hata hoja za kuzungumza ndani ya Bunge.

“Nimewahi kuulizwa mara kadhaa mbona huna kesi, mbona huko mahakamani? Hili ni swali ka kumuuliza ina maana wanataka nikisimama niwe mtukanaji, niwe lopolopo na niwe na kesi za ajabu ajabu.

“Nimekataa haya mambo ya ndimi mbili linalotoka mdomoni silo lililopo moyoni, kila kukicha wanazusha uongo kupaka watu matope,” alisema.

Alisema amesoma alama za nyakati kwa upinzani uliyopo wa ghiliba, nongwa na watu walewale watasubiri sana wanaouunga mkono kwa sababu hakuna upinzani nchini ni unafiki tu.

Chanzo: mwananchi.co.tz