Dodoma. Baadhi ya wabunge wa upinzani leo Jumatano Novemba 6, 2019 wamelitaka Bunge la Tanzania kusitisha shughuli zake ili kujadili hali ya sintofahamu iliyojitokeza wakati wa kurejesha fomu za uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Vyama vya upinzani vimelalamikia ukiukwaji wa kanuni na kufanyiwa hujuma zilizosababisha kuenguliwa kwa wagombea wao wengi kwenye mchakato wa uchaguzi huo.
Uchaguzi wa Serikali za mitaa utafanyika Novemba 24, 2019 na hatua ya uchukuaji fomu kwa wagombea ilimalizika Novemba 4, 2019.
Nafasi zinazowaniwa ni mwenyekiti wa kitongoji, mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na wajumbe wa kamati ya mtaa.
Waliozungumzia sintofahamu hiyo bungeni leo ni Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini), Magdalena Sakaya (Kaliua), Frank Mwakajoka (Tunduma) na Anatropia Theonist
Mwakajoka amesema kinachoendelea kuhusu uchaguzi huo kinaweza kusababisha machafuko na uvunjifu wa amani kama Serikali haitakuwa makini.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Jafo ataka walioenguliwa uchaguzi Serikali za mitaa kurejeshwa
- VIDEO: Chadema yaitisha vikao vya dharura kuenguliwa wagombea wao serikali za mitaa kila kona
- Matumizi ya R na L yawachanganya wapinzani uchaguzi serikali za mitaa
- Mbatia: Wagombea wote wa NCCR jimbo la Vunjo wameenguliwa
Maftaha amesema wana vielelezo vya kanuni zilizokiukwa katika uchukuaji wa fomu za uchaguzi huo na kuomba avikabidhi kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ili chombo hicho cha Dola kisitishe shughuli zake, kujadili uchaguzi huo.
Akijibu miongozo hiyo naibu spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge kuwa wavumilivu kwa maelezo kuwa Jafo alishatoa maelekezo yanafanyiwa kazi.