Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapinzani walishindwa uchaguzi tangu siku ya kwanza ya kampeni

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita Agosti 12 katika Jimbo la Buyungu na kata 77 nchini ulionekana wazi kuvielemea vyama vya upinzani. CCM ilishajinyakuliwa keki yote tangu siku ya kwanza.

Kwenye uchaguzi huo, CCM imezoa kata zote 77 ambapo kata 41 kati ya hizo ilipita bila kupingwa, huku pia ikichukua jimbo la Buyungu mkoani Kigoma.

Jimbo la Buyungu mgombea wa CCM Christopher Chiza alipata kura 24,578 akifuatiwa na mgombea wa Chadema aliyepata kura 16,910.

Vyama vingine vilivyoshiriki ni pamoja na Demokrasia Makini kilichopata kura 11, UMD 12, NRA 17, UPDP 18, DP 22, AFP 51 na ACT - Wazalendo 100.

Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, Lusubilo Mwakabibi, idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ni 61,980, waliopiga kura ni watu 42,356, kura halali 41,841 na kura zilizoharibika ni 515.

Hayo ndiyo matokeo yaliyowaacha wapinzani vinywa wazi, ingawa walijua kuwa ni vigumu kupata ushindi, huku CCM ikichekelea ushindi.

Wagombea upinzani waenguliwa

Dalili za wapinzani kushindwa zilianza tangu wakati wa kuwapata wagombea, ambapo wengi kutoka upinzani walienguliwa na mamlaka za kusimamia uchaguzi na kuwaacha wa CCM wakipita bila kupingwa.

Hadi siku ya uteuzi wagombea 30 wa CCM katika kata 77 walikuwa wameshatawazwa kuwa madiwani. Baada ya kusikiliza rufaa na matukio mengine ya wagombea kujitoa. Chama hicho tawala kilifikisha madiwani 41 kabla ya kufika katika sanduku la kura. Hizo zilikuwa dalili za wazi kuwa chama hicho kingeibuka kidedea katika sehemu zote.

Hatua hizo za kupita bila kupingwa, wapinzani hasa Chadema wanadai nguvu za dola zilitumika. Kwa mfano, baadhi ya viongozi wa chama hicho Tunduma mkoani Songwe walidaiwa kukimbilia mafichoni wakihofia kukamatwa, huku mbunge wa jimbo hilo (Chadema), Frank Mwakajoka akishikiliwa na polisi na baadaye kuachiwa.

Akieleza hali ilivyokuwa katika uchaguzi huo katika Mkoa wa Songwe, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Sofia Mwakagenda anasema wagombea wao walinyanyaswa.

“Kwa mfano kule Tunduma kuna vijana watano wa Chadema, jioni tumefanya uchaguzi, asubuhi polisi wamekwenda kwa madiwani wale, mmoja akaambiwa wewe unazuia TRA wasikusanye kodi. Mwingine anaambiwa kwamba wewe ulitaka uue mtu saa sita usiku,” anadai Mwakagenda.

Anasema katika jimbo la Mbozi, msimamizi wa uchaguzi alikataa wagombea halali wa Chadema na kuweka wagombea wasiojulikana kupitia chama hicho.

“Saa sita mchana, tukiwa kwenye kesi ya mbunge Haonga, vijana wetu wakiwa wameshajaza fomu, wanazipeleka kwa kiongozi wa Tume, msimamizi anasema mimi nimeshapata watu wa Chadema, fomu zimeshaletwa. Tunajiuliza, watu wa Chadema? Ni kina nani? Majina hayajulikani, hayapo na msimamizi anang’ang’ania.

“Sheria ya uchaguzi inasema, kama ngazi ya wilaya imeshapeleka majina na mkoa ambayo ndiyo ngazi ya juu inaweza kutengua hayo majina. Kamati Kuu ikaamua katibu mkuu apeleke barua ya wagombea anaowatambua yeye. Msimamizi akakataa. Sasa huu ndiyo uhuni ambao hatupendi utufikishe pabaya.”

Ukiacha Chadema, Katibu wa Itikadi, mawasiliano na uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alinukuliwa hivi karibuni akisema kati ya wagombea 15 wa chama hicho waliorejesha fomu, wanne walienguliwa.

Wagombea wanne wamefanyiwa vitimbi na kuenguliwa. Wagombea watatu katika kata zilizopo Tunduma hawakuteuliwa kwa kigezo kwamba si raia,” anasema Shaibu.

Wapinzani hawakuishia tu kulalamika bali, walipeleka malalamiko yao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia rufaa 25 za kupinga kuenguliwa.

Mkurugenzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia anasema Tume ilipokea rufaa 25 ambazo walizifanyia kazi kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na kuwarejesha wagombea 10 kati ya hizo.

Hatua hiyo ya kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani imeibua maswali kadha ikiwamo kutoenguliwa kwa wagombea wa CCM kana kwamba hawajawahi kukosea tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze.

Swali lingine linawahusu wasimamizi wa uchaguzi ambao ni Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya (DEDs) ambao ni wateule wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ambayo wagombea wake ndio wanapita bila kupingwa.

Swali pia linaihusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo uongozi wake umeteuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM. Ni kwa kiasi gani Tume hiyo iko huru kutenda haki bila kukwaza wenye mamlaka.

Kampeni

Mbali na wagombea wa upinzani kuenguliwa, viongozi wa vyama hivyo hawakuweka nguvu kubwa kwenye kampeni tofauti na CCM iliyotumia wabunge, viongozi wastaafu, mawaziri na wengineo kujinadi.

Baadhi ya viongozi wa upinzani hasa wa Chadema akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, John Mnyika (Kibamba), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar), Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe) na Peter Msigwa (Iringa Mjini) wamekuwa wakitumia muda mwingi kuhudhuria kesi zinazowakabili mahakamani na mara chache tu kujikita kwenye kampeni.

Miongoni mwa kata zilizokuwa na upinzani mkali katika uchaguzi huo ni Turwa wilayani Tarime, Mara ambapo msimamizi msaidizi wa uchaguzi alivizuia vyama vya upinzani kufanya kampeni kwa siku kadhaa na kuiacha CCM pekee ikitamba.

Katika barua yake iliyosambaa mitandaoni, msimamizi huyo alisitisha mikutano yote ya kampeni ya vyama vya upinzani kwenye kata hiyo.

Taarifa hizo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii kupitia barua inayodaiwa kutolewa na msimamizi, Peter Julius alisitisha kampeni kwa chama cha NCCR Mageuzi Agosti 10, 2018 hadi Agosti 11, 2018.

Sehemu ya barua hiyo inaeleza kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya NCCR-Mageuzi kudaiwa kukiuka sheria ya taifa ya uchaguzi.

“Nakujulisha kwa kufuatia chama tajwa hapo juu kukiuka kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Kata ya Turwa kupitia kikao kilichoketi tarehe 10/08/2018 kimesitisha kampeni za chama hicho kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 10/08/2018 hadi 11/08/2018,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Kabla ya NCCR-Mageuzi kusitishwa kufanya kampeni kata ya Turwa, Chadema pia ilisitishwa kufanya kampeni za udiwani kwenye kata hiyo.

Nguvu ya Polisi

Siku chache kabla ya kuisha kwa muda wa kampeni, Jeshi la Polisi mkoani Mara liliwatawanya viongozi na wafuasi vyama vya upinzani katika Kata ya Turwa wilayani Tarime na kumkamata Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na watu 10 akiwemo mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma na kuwashikilia kwa simu moja.

Hata hivyo, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyekuwapo kwenye eneo hilo alisema vyama hivyo vitaendelea na kampeni kwenye maeneo mengine.

Vurugu

Vurugu zilijidhihirisha siku ya uchaguzi jijini Arusha baada ya watu wawili kujeruhiwa akiwamo mgombea udiwani wa kata hiyo, Boniface Kimario na wakala wale Ibrahim Ismail kuchomwa visu huku mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema akishambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa walinzi wa CCM.

Jeshi la Polisi mkoani humo limekiri kuwa na taarifa za vurugu hizo likisema limefungua jalada la uchunguzi na hadi sasa haijulikani kama hatua zaidi zimechukuliwa.

Kicheko CCM

Akizungumzia siri ya ushindi wa CCM Jumatatu katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally anasema chama hicho kimewapa matumaini wananchi kiasi cha kuaminika na hivyo kushinda uchaguzi huo.

“Ninashawishika kusema tumeanza kufanya kazi inawapa watu matumaini hasa wanyonge. Kila tulipopita tunazungumza lugha za matumaini na pengine tukikuta kero tunatatua,” anasema Dk Bashiru.

Ametaja pia siri ya kuwatumia viongozi wastaafu akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba.

“Tumefanya mikutano ya nje na ndani. Mimi nimefanya mikutano 25 ya ndani, nimezungumza na viongozi wa dini 11 na mtu mmoja mmoja,” anasema.

Kuhusu vyama vya upinzani, Dk Bashiru anasema hawakuwa wamejipanga badala yake waliishia kupiga porojo kwenye mitandao ya kijamii.

“Ni wakati muhimu kujiuliza, ni aina gani ya siasa tunazofanya. Tujiulize ni wapi tulipotoka tunapokwenda. Napenda kuwashukuru Watanzania kwa imani yao na tutaitumia kuwalipa. Hatutadeka wala kubweteka.”

Kauli za wagombea

Wagombea wawili waliopata kura za juu kutoka CCM na Chadema walikuwa kauli za kutia faraja baada ya kupokea matokeo hayo.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi wa jimbo hilo, Chiza aliyewahi pia kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili, anasema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo na kuwaahidi utumishi uliotukuka.

“Kazi ya mbunge ni kujua matatizo ya wananchi na kuhakikisha anayafikisha kwa wale wanaoweza kutatua matatizo hayo na kurejesha majibu anayoyapata kwa wapiga kura huko anakopeleka matatizo,” amesisitiza.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa Chadema, Elia Kanjero amesema uchaguzi huo umemjenga kisiasa na anazichukulia changamoto za uchaguzi huo kama mafunzo kwa chaguzi nyingine.

“Nimejifunza kutokana na uchaguzi na umenijenga kwa kiwango kikubwa, ninashukuru kwamba nimepewa fursa ya kushiriki, miaka mingine tutaonana umri bado unaruhusu,” anasema na kuongeza;

“Kwa kuwa mimi bado ni kijana yote nayachukua kama changamoto, yananijenga mimi. Siko tayari kupambana kwa ajili ya madaraka. Nimemaliza uchaguzi salama na umenijenga kwa miaka mingine.”

Chanzo: mwananchi.co.tz